SAMATTA: NITAMSHAURI MWALIMU NA BENCHI LA UFUNDI TUTUMIE NJIA GANI KUPATA MAGOLI DHIDI YA ALGERIA


 
Mbwana Samata
Mbwana Samata

Mshambuliaji nyota wa Tanzania Mbwana Samatta, yupo Algeria na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya kupambana na Algeria 'Mbweha wa Jangwani' kwenye mchezo wa marudioano kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la duni za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Urusi.

Samatta alikuwepo Algeria majuma kadhaa yaliyopita akiwa na klabu yake ya TP Mazembe kucheza mchezo wa awali wa fainali ya klabu bingwa Afrika dhidi ya timu ya USM Alger ya Algeria mchezo uliomalizika kwa Mazembe kupata ushindi wa goli 2-1 huku Samatta akifunga goli la pili kwa upande wa klabu yake kwa mkwaju wa penati.

Yahaya Mohamed ambaye amesafiri na kikosi cha Stars hadi nchi Algeria amefanya mahojiano na Samatta akitaka kujua kama kuna faida ya Samatta kucheza dhidi ya klabu ya Algeria kwenye mchezo wa kwanza wa fainali ya klabu bingwa Afrika uliochezwa nchini umo kuelekea kwenye mchezo wa leo kati ya Taifa Stars dhidi ya Algeria.

"Mimi naona sisi tunatakiwa kupata magoli kwasababu ndiyo jambo la muhimu, sare yoyote kwetu ya goli 1-1 au ya bila kufungana haitusaidii, tunachoangalia sasahivi ni njia ya kupata magoli na njia hiyo naiona na nitajaribu kumshauri mwalimu na benchi la ufundi tuone tunafanyaje kuweza kupata magoli kwasababu tunaweza kufunga nauhakika na hilo kwa 100%", Samatta alisema kwa kujiamini huku akionekana mwenye matumaini makubwa kuelekea kwenye mchezo huo.

Samatta alifunga goli la pili kwenye mchezo wa awali uliofanyika jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita November 14, 2015 wakati Maguli alifunga goli la kwanza kwenye mchezo uliomalizika kwa Stars kulazimishwa sare ya kufungana magoli 2-2 na Algeria.



Comments