MWAKA MMOJA WA HASSAN KESSY SIMBA SC HAIJAFIKIA HATA THAMANI ALIYOSAJILIWA..HANA THAMANI YA MILIONI 45 KWA SASA


MWAKA MMOJA WA HASSAN KESSY SIMBA SC HAIJAFIKIA HATA THAMANI ALIYOSAJILIWA..HANA THAMANI YA MILIONI 45 KWA SASA

KK

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Miezi 11 iliyopita Simba SC ilimsaini mlinzi wa kulia, Ramadhani Kessy kutoka klabu bingwa mara mbili ya zamani ya Tanzania bara, Mtibwa Sugar. Kessy alikuwa na misimu miwili ya kupenda katika timu ya Mtibwa chini ya kocha Mecky Mexime ambaye alimpandisha kikosi cha kwanza kijana huyo 'zao' la timu ya vijana ya Moro Kids msimu wa 2013/14.

Uwezo wake wa kukaba, kuzuia mashambulizi, kupandisha timu kwa kasi na kupiga krosi ulimtambulisha Kessy kama 'namba 2 wa kupanda na kushuka'. Simba ilimsaini kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu na mchezaji huyo alitia saini baada ya kukubali makubaliano ya kupewa zaidi ya milion 20.

Kwanza, nawalaumu Simba kwa kuwa walifanya makosa kumpatia kijana huyo mkataba mfupi wakati ni mmoja kati ya walinzi bora wa kulia kwa sasa Tanzania. Pili, napenda kumshauri Kessy kufikiria mara mbili kuhusu atma yake ya siku za usoni katika uchezaji wake.

Kessy ametamka wazi kuwa 'dau lake kwa sasa halipungui milion 45', anamaanisha kuwa timu itakayokuwa tayari kumpatia pesa hiyo ndiyo ataichezea mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa sasa.

Ajifunze kwa Himid, Bocco, Salum, Ndemla….

Himid Mao, John Bocco, Salum Abubakar hawa ni vijana ambao wameonesha ukomavu mkubwa kifikra. Wamedumu ndani ya Azam FC tangu msimu wa kwanza wa timu hiyo katika ligi kuu takribani miaka 8 iliyopita.

Si kwamba, uwepo wao ndani ya Azam FC hadi sasa umekosa changamoto. Walilazimika kushindana na wachezaji wengi wa ndani ya nchi na nje ambao walijiunga na timu hiyo tajiri zaidi Tanzania. Walipambana na wamejikuta wakiwa sehemu ya historia ya kukumbukwa miaka yote ya klabu hiyo. Wakati fulani walijikuta wakikosa nafasi kikosi cha kwanza ila wakaendelea kuwa wavumilivu na kupigania nafasi.

Walishuhudia wachezaji wengi wakija na kupewa mishahara mikubwa zaidi yao lakini waliendelea kucheza kwa moyo na kuisaidia timu yao. Hakika ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wengi vijana nchini ambao wanashindwa kucheza na alama za nyakati.

Mchezaji pekee kuzifunga mara nyingi zaidi timu kubwa za Yanga SC na Simba SC katika historia ya nchi hii ni Bocco, na alikuwa na nafasi ya kuchagua kujiunga na moja ya timu hizo au kuzichezea zote kwa nyakati tofauti katika misimu yake nane VPL, Himid ni mchezaji pekee wa nafasi ya kiungo kucheza misimu mitatu mfululizo kwa kiwango cha juu. Vipi kuhusu kipaji cha Salum ambacho kiliwapagawisha Simba na Yanga?

Lakini wote watatu 'wameridhika', wamecheza ligi kuu michezo mingi pengine kuliko wachezaji wote katika misimu 7 iliyopita. Said Ndemla, huyu pia ni mfano mzuri kwa mchezaji kinaja ambaye anatazama fedha na maendeleo yake kiuchezaji. Alikuwa na chaguo la kujiunga na klabu yoyote Tanzania katikati ya mwaka huu lakini akaichagua tena Simba mara baada ya mkataba wake wa awali kumalizika.

Ndemla hakujitangaza thamani yake na pengine angesaini mkataba mpya hata kwa milion 25 achilia mbali 30 ambazo walikubaliana na timu yake ambayo ilimpandisha kutoka timu yao ya vijana miaka minne mitatu iliyopita.

Kessy hawezi kupewa zaidi ya milion 30 na Simba labda aisaidie timu hiyo kushinda ubingwa au kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Caf. Hajafanya chochote cha ajabu tangu akiposaini mkataba wa kwanza Disemba mwaka jana.

KIUCHEZAJI SIMBA PANAMFAA ZAIDI, KIMASLAI, KESSY AENDE YANGA, AZAM.

Si 'taipu' ya Yanga kiuchezaji, hawezi kupata nafasi mbele ya Shomari Kapombe pale Azam FC. Nini kitafuata kwa Kessy ikiwa atajiunga na timu mojawapo kati ya hizo mbili.? Hassan Dilunga, Hussein Javu walifanya anachojaribu kutaka kufanya Kessy, walichemsha vibaya ndani ya Yanga sasa wanajaribu 'kufufuka' Stand United ( Dilunga), Mtibwa Sugar ( Javu).

Hussen Sharrif pia ni mfano wa mchezaji aliyefuata zaidi fedha kuliko maendeleo yake kiuchezaji baada ya kuachana na Mtibwa na kujiunga na Simba katikati ya mwaka uliopita. Kessy aende tu pale anapotaka ila Simba hawawezi kumsaini kwa dau analotaka sasa ndani ya muda mfupi tangu wampe kiasi kikubwa cha pesa. Aisaidie kwanza timu kushinda ubingwa ili thamani yake ipande zaidi.

Mwaka mmoja wa Hassan Kessy Simba SC hajafikia hata thamani aliyosajiliwa! Hana thamani ya milion 45 kwa sasa, labda Simba itwae ubingwa msimu huu thamani yake itapandishwa na mafanikio. Msimu mmoja au miwili zaidi Kessy anapaswa kucheza mfululizo ndani ya Simba pekee ndiyo anaweza kupata nafasi hiyo. Yanga na Azam sasa kuna ' majembe' si rahisi kwake. Alishinda vita ya namba dhidi ya kapteni Nassoro Chollo ila usiniambie anaweza vita dhidi ya Mbuyu Tite, Juma Abdul na Kapombe!



Comments