MAGULI AFURAHIA KUCHEZA NA SAMATTA


MAGULI AFURAHIA KUCHEZA NA SAMATTA

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania Elius Maguli              akishangilia baada ya kufunga goli la kwanza

Kinara wa upachikaji mabao wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara Elius Maguli ambaye amerejea kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Stars tangu alipoachwa kwa mara ya mwisho mwaka 2013. Maguli alianza kwenye kikosi cha kwanza kwenye mchezo dhidi ya Algeria uliochezwa jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kufunga goli la kwanza kwenye sare ya kufungana magoli 2-2.

Mtandao huu umetaka kujua Maguli alijisikiaje kurejea tena kwenye kikosi cha Stars na kupata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

"Kwangu mimi ni furaha kwanza ukizingatia mwalimu aliniamini na kunipa nafasi, ikabidi na mimi nijiamini ili niweze kufanya vizuri kama ilivyoweza kutokea", alisema Maguli wakati akizungumza na Yahaya Mohamed kabla ya mazoezi ya jana usiku kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Algeria utakaochezwa leo saa tatu usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Maguli alipoulizwa anajisikiaje kusimama mbele kwenye nafasi ya ushambuliaji pamoja na Mbwana Samatta kwenye kikosi cha Stars alisema kwamba, anafurahi kucheza na Samatta na ushirikiano ndiyo ulizaa mabao mawili kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Algeria.

"Ushirikiano ni mzuri, kabla ya mchezo tuliocheza nyumbani kuanza, tulikaa na kuzungumza ni kitu gani tufanye ili tuweze kupata magoli na kilichotokea ni kile ambacho kila mtu aliona".

Maguli alionesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa awali uliochezwa jijini Dar es Salaam na huenda leo akawa miongoni mwa wachezaji ambao wataanza kwenye kikosi cha kwanza wakati Stars itakapokuwa ikikabiliana na Algeria kwenye mchezo wa marudiano.



Comments