Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Mshambulizi wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ' Samagoal' atajiunga na timu ya ligi kuu ya Ufaransa, Lille mara baada ya kutimiza ndoto zake za miaka mitatu iliyopita ya kucheza klabu bingwa ya dunia. Mfungaji huyo bora wa ligi ya mabingwa Afrika 2015 ambaye amefunga magoli 8 katika mechi kumi na ku-assist mara tatu ataichezea Mazembe kwa mara ya mwisho katika michuano hiyo na kutimkia ulaya
Mshambulizi huyo wa Taifa Stars ambaye alitwaa tuzo ya mfungaji wa ligi ya mabingwa Afrika wikendi iliyopita na kushinda pia ubingwa wa michuano hiyo aliniambia kwa mara ya kwanza miaka mitatu iliyopita kuwa atahakikisha anaipa ubingwa TP ili kucheza michuano klabu duniani ambayo itafanyika nchini Japan mwezi ujao wa Disemba.
Samatta ni kijana ambaye alianzia maisha yake ya soka la ushindani katika timu ya Mbagala Market ( African Lyon) mwaka 2009. Alifunga magoli 15 katika ligi daraja la kwanza na kuisaidia timu yake kupanda ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2009/10.
Alifunga magoli sita katika msimu wake wa ligi kuu Bara akiwa kinda wa miaka 17 na mara baada ya kumalizika kwa msimu alisajiliwa Simba SC ambayo aliichezea kwa miezi mitatu tu- Januari-April, 2011 alipouzwa TP Mazembe kwa ada ya rekodi wakati huo milioni 150.
Katika mechi yake ya kwanza tu alifunga ' Hat-Trick' akiwa na timu hiyo ya DRC na akawa mmoja wa wachezaji maarufu zaidi jijini Lubumbashi. Rekodi yake ya ufungaji inajieleza yenyewe na kumtambulisha kama ' goal machine'. Aliichezea Simba mara 25 tu na kutumbukiza nyavuni magoli 13 yakiwemo matatu katika ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2011
Amecheza kwa misimu minne katika klabu ya TP Mazembe na licha ya kuhitajika mno katika timu hiyo ya DRC, Samatta amekuwa kwa misimu miwili sasa akisisitiza kutaka kwenda barani ulaya. Mara kadhaa amesisitiza kuwa inatosha kwa yeye kuendelea kucheza barani Afrika.
Kuna wakati alipofanya mahojiano na Shirika la utangazaji la Uingeeza, BBC alinukuliwa akisema kuwa " sijui kwa nini hatuna mchezaji anayecheza barani ulaya, naamini nitakuwa mmoja wao"
Kiwango chake katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika msimu uliolizika wiki iliyopita kimemfanya kuwa miongoni mwa wachezaji 10 bora wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika 2015 kwa wale wanaocheza ndani ya Afrika.
Katika mchezo wa kwanza wa fainali dhidi ya USM Algers ugenini alifunga goli la mkwaju wa penalty. Na katika gemu ya marejeano kijana huyo mwenye miaka 22 alifunga tena goli la mkwaju wa penalty na hivyo kufikisha magoli nane na kutwaa kiatu cha dhahabu.
Amekuwa mcheza-soka wa kwanza wa Tanzania kushinda tuzo hiyo huku yeye na rafiki yake Thomas Ulimwengu wakiweka rekodi ya kuwa Watanzania wa kwanza kucheza mechi ya fainali ya klabu bingwa Afrika, pia wamekuwa Watanzania wa kwanza kushinda ubingwa huo.
Ni mafanikio ' bab-kubwa' ambayo sit u yamemtoa machozi ya furaha baba yake mzazi ' Mzee Ally Samatta' bali yametazamwa na Watanzania wengi kama ' fahari na kielelezo' cha vipaji vingi vilivyopo nchini.
"Nilifurahi sana baada ya kumuona akishangalia goli lake la nane kwa kuipeperusha bendera ya Tanzania. Anaonyesha sasa Tanzania inapepea na jinsi gani anaipenda nchi yake. Namuheshimu sana na najivunia. Sasa tunaanza kutambulika katika dunia na milango zaidi itafunguka kwa wachezaji wetu" anasema msomaji wa Mtandao huu, Sulleyman Jimmy
"Ni sifa kubwa kwa taifa letu, lakini pia ni wakati wake wa kusonga mbele zaidi kwa kuwa anastahili kwenda mbali sasa" Said Madandi anasema msomaji mwingine wa mtandao huu. Samatta anatazamiwa kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza moja ya ligi kubwa tano za ulaya mara baada ya kujiunga na Lille. Huu ni wakati ambao kila Mtanzania nasisimka kusika habari zake za kwenda ulaya.
Comments
Post a Comment