KOCHA mkuu wa England, Roy Hodgson amewataka wachezaji wa timu hiyo kutovurugwa na kichapo cha juzi kutoka kwa Hispania, ambacho ni cha kwanza katika miezi 17 iliyopita.
England ambayo haijapoteza mchezo wowote katika michezo ya kufuzu mashindano ya Euro 2016, ilikumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Hispania katika mchezo wa kirafiki, huku mabao hayo yakitupiwa wavuni na Mario Gaspar na Santi Cazorla.
Hata hivyo, Hodgoson aliitaka timu hiyo kuachana na matokeo hayo na badala yake kuhakikisha haipotezi hali ya kujiamini na kufanya vizuri katika michezo ijayo.
"Unapopoteza mchezo kwa mara ya kwanza, jambo muhimu ni kuhakikisha haupotezi hali ya kujiamini," alisema Mwingereza huyo.
Kikosi hicho kilishuka dimbani bila ya kinara wa mabao Premier League, Jamie Vardy ambaye ni majeruhi na anaweza kukosa pambano dhidi ya Ufaransa, mchezo utakaochezwa kesho kwenye dimba la France Wembley Stadium nchini England.
Comments
Post a Comment