STAA wa Manchester United, Juan Mata, amemshauri nyota mwenzake, Memphis Depay kuendelea kubaki kwenye klabu hiyo akisema kuwa hana wasiwasi kama straika huyo atashindwa kung'ara akiwa Old Trafford.
Msimu uliopita Memphis (pichani juu) aling'ara kwenye Ligi ya Uholanzi ambapo alifunga mabao 22 katika msimu ambao PSV walitwaa ubingwa, huku akionyesha kiwango cha hali ya juu.
Hata hivyo, nyota huyo wa timu ya taifa ya Uholanzi, ameshindwa kung'ara katika mashindano ya Ligi Kuu tangu aliposajiliwa na Manchester United kwa ada ya pauni mil. 19.3.
Kutokana na hali hiyo, Mata ameamua kumpa darasa akisema kuwa Depay anatakiwa kuwa mvumilivu ili kuondokana na hali inayomkabili.
"Memphis licha ya kutofanya vizuri akiwa na Man United, lakini msimu uliopita alikuwa tishio aiwa na PSV na nadhani ndio maana akawamo kwenye orodha ya wachezaji 50 bora.
"Amewahi kufunga mabao mengi na kuna mazuri yapo mbele yake. Hajacheza mara nyingi lakini anatakiwa kuwa na subira kwasababu bado ni kijana mdogo na mwenye ipaji kikubwa," alisema staa huyo Mhispania.
Comments
Post a Comment