DOYE MOKE : BARTHEZ ALIKUA MZEMBE, STARS INAHITAJI WACHEZAJI WA KIMATAIFA ZAIDI


DOYE MOKE : BARTHEZ ALIKUA MZEMBE, STARS INAHITAJI WACHEZAJI WA KIMATAIFA ZAIDI

BBN Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Baada ya kushuhudia timu ya kandanda ya Tanzania ikichapwa kipigo 'kikubwa zaidi' tangu ilipojiunga FIFA mwaka 1964, wadau mbalimbali wamejitokeza na kuweka wazi hisia zao. Taifa Stars ilifungwa 7-0 na Algeria usiku wa jana Jumanne ikicheza ugenini na hivyo kuondolewa katika hatua ya pili kuwania kufuzu kwa hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za kombe la dunia nchini Urussi.

Kipigo cha jumla cha mabao 9-2 kimewaacha 'wazi' kila mmoja na sasa naamini Tanzania ina safari ndefu kufikia kufuzu kwa michuano mikubwa. Mara ya mwisho kwa Stars kufuzu kwa fainali kubwa ni mwaka 1980 katika fainali za mataifa ya Afrika nchini Nigeria. Baada ya hapo, kizazi hadi kizazi hakuna kipya walichoweza kufanya.

Kufuzu kwa CHAN 2009 michuano ya kwanza kwa Mataifa ya Afrika inayohusisha wachezaji wa ndani ya Afrika pekee ilikuwa ni kama 'bahati ya mtende' lakini ghafla timu haikudumu katika ubora wake na ikapotelea mbali.

Kizazi hiki cha sasa ambacho kinawajumuhisha washindi pekee wa klabu bingwa Afrika, Thomas Ulimwengu na mfungaji bora wa michuano ya klabu Afrika, Mbwana Samatta ndiyo kimejikuta katika historia mbaya zaidi kimpira.

Hakuna unachoweza kusema sasa, labda ni kukubali tu udhaifu wa ligi kuu ya Tanzania bara ambayo 'watawala' wake Yanga SC, Azam FC na Simba SC ndiyo wamekuwa wakiunda sehemu kubwa ya timu ya Taifa. Wakati huu wachezaji wa Kitanzania wakiwa wameanza kutawanyika nje ya mipaka ya nchi, maofisa wa TFF na wakufuzi wa timu wameshindwa kuhakikisha wanapatikana wakati Stars inapobaliwa na gemu za kimataifa.

Abdi Kassim, Hamis Mroki, Juma Ndanda Luinzo, Uhuru Suleiman, Mrisho Ngassa, Ulimwengu na Samatta hawa ni baadhi wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje ya nchi lakini ni watatu tu wanaojumuhishwa katika timu. TFF na walimu wanaamini kuwa wachezaji wanaocheza VPL ni wazuri zaidi lakini mpira wa kimataifa unahitaji pia mbinu mpya kiuchezaji kila wakati hasa kwa wachezaji.

Kama tunahitaji vijana watu waende kucheza nje ya nchi basi tuwe tayari pia kuwaita katika timu ya Taifa kwa kuwa ni sifa pia kwa mchezaji klabuni kwake, inamuongezea uwezo, heshima na msaada wake uwanjani huwa mkubwa kuliko mchezaji bora wa VPL.

"Mimi binafsi nafahamu kiundani soka la bongo, katika ufahamu wangu, mchezaji wa kibongo au coach wa kibongo wanatabia moja. M-bongo akiwa ndani ya Tanzania ni mjanja kwa kila kitu, akitoka nje ya Tanzania anakua mdogo sana kwa kila kitu." Anaanza kusema mlinda mlango wa zamani wa Simba SC na Yanga SC , Doy Moke

"Taifa Stars ilipoteza mchezo kutokana na kutokujiamini, woga, hasa mimi binafsi lawama zote na mpa Barthez (kipa Ally Mustapha) kwa kufungwa magoli ya kizembe mno hasa dakika ya kwanza. Kwa uzoefu wangu timu ilicheza ugenini mwenye jukumu la kuibeba timu ni kipa anapaswa kucheza zaidi ya asilimia 60 kwa kuibeba timu na kuwapanga mabeki wake".

"Nakumbuka nilivyokua Yanga mwaka 2001 tulienda Bulawayo kucheza ugenini kabla ya mechi kuanza kila mchezaji wetu alipanic, Mahadhi akanifata na kuniomba tusifungwe magoli mengi, bora nijitahidi tufungwe machache, nilivyo mtazama usoni nikaona alikua akitetemeka.

"Nilimwambia hakika hatutafungwa hâta goli 1, hakuniamini, lakini game ilivyo anza walitushambulia kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya ishirini niliokoa hatari zote kwa ujasiri, timu yote ikajenga imani kwangu, nakurudi katika game, mwisho tulishinda 2-0 ugenini." Anasimulia Moke

"Wachezaji wengi wa kibongo huchukulia mpira kama mwajiriwa wa kampuni fulani, hana mpango wakujiendeleza, bora afanye mazoezi na aoneshe nidhamu basi. Football ni zaidi ya hiyo. Kuletwa kwa wachezaji wakigeni kumeifanya Tanzania angalau mpira uanze kuchezwa, lakini kwa wachezaji wakibongo wanaocheza VPL safari bado ni ndefu mno kwao.

"Niliona hayo ujasiri wa timu ya taïfa ya Burundi (Jumatatu hii) walicheza mbele ya watu laki moja (100,000) uwanjani wa Stade de Martyrs, Kinshasa, walicheza vizuri mno nakuunyamazisha umati mkubwa kwa kupata matokeo ya goli 2-2 ugenini.

"Kwa Tanzania bora wachezaji wa cheze nje ya Tanzania, na ma-coach hivyo hivyo. Bila hivyo mh!, Yanga kabla hawajaingia Champions Leagues watafute golikipa jasiri, bila ivyo itakua kazi bure".



Comments