DE GEA KWENYE MTIHANI MZITO, REAL MADRID KULIANZISHA TENA


DE GEA KWENYE MTIHANI MZITO, REAL MADRID KULIANZISHA TENA

WAKATI Manchester United wakionekana kutaka kutulia na kuelekeza nguvu kwenye mipango ya kujiimarisha zaidi,  Real Madrid inaanza kuwachanganya.

Kuelekea dirisha la usajili wa Januari, klabu hiyo imeanza tena kusambaza fitna na sumu mbaya kwa kusema itamsajili kipa David De Gea, katika dirisha hilo la usajili.

Taarifa hizo ni mbaya mno masikioni mwa mashabiki wa United kutokana na umuhimnu wa kipa huyo aliye chaguo la kwanza.

De Gea ambae alikwama kuihama timu hiyo katika siku ya mwisho ya usajili wa kiangazi kutokana na kilichoelezwa kuwa ni uzembe, alishabainisha kuwa ana mapenzi na Real Madrid.

Kocha Louis Van Gaal, alishamruhusu kipa huyo kuhama, lakini baada ya dili hilo kushindikana alimsihi arejeshe moyo na kuitumikia United.

Taarifa za Real Madrid zimetiwa nguvu na rais wa Ligi Kuu ya Hispania 'La Liga', Javier Tebas ambae alinukuliwa juzi, alisema anaziona dalili za De Gea kukipiga katika Ligi hiyo.

"Sio siri, ingawa De Gea amesaini mkataba mpya wa kuitumikia Manchester United, bado sidhani kama hiyo itafanya abaki huko milele," alisema.

Aliongeza kusema, kila klabu inahitaji kuwa na kipa bora kama David De Gea, lakini kutokana na ukweli kuwa uyo ni mzaliwa wa Hispania, basi ana nafasi kubwa ya kukipiga nchini humo.

Aliifagilia La Liga akisema ni moja ya Ligi bora zaidi Ulaya katika miaka hii na ushahidi ni jinsi klabu za nchi hiyo zinavyotawala soka la michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europe League.

Aliongeza kusema kuwa, hajali iwapo kipa uyo atachelewa kurudi Hispania, lakini alicho na matumaini nacho ni kuwa, hata De Gea mwenyewe anatamani sana kuanza kukipiga katika Ligi hiyo.


Comments