ALGERIA YAIFUNGASHIA STARS FURUSHI LA MAGOLI



ALGERIA YAIFUNGASHIA STARS FURUSHI LA MAGOLI
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'
Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'

Timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imeondoshwa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kupangwa kwenye hatua ya makundi kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia mwaka 2018 ambazo zitafanyika nchini Urusi baada ya kufungwa kwa magoli 7-0 kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye uwanja wa Mustapher Tchaker mjini Blida, Algeria

Stars imeondoshwa kwa jumla ya mabao 9-2 baada ya kucheza michezo miwili, mchezo wa kwanza Stars ililazimishwa sare ya kufungana kwa goli 2-2 na Algeria jijini Dar es Salaam huku mchezo wa pili uliopigwa Blida, Algeria ukimalizika kwa Stars kulala kwa goli 7-0.

Algeria walianza kupata bao la kwanza sekunde ya 40 kupitia kwa Yacine Brahimi huku Ghoulam Faouzi akipachika goli la pili dakika ya 23 kabla ya Ryad Mahrez kutupia la tatu dakika ya 43 na kuufanya mchezo kwenda mapumziko Algeria wakiwa mbele kwa magoli 3-0 dhidi ya Stars.

Kipindi cha pili kilianza kwa Stars kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Farid Musa na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Telela wakati Aishi Manula aliingia kuchukua nafasi ya Ali Mustafa.

Dakika ya 49 Algeria waliendeleza mvua ya magoli kwa Stars baada ya Slimani Islam kuipatia Algeria bao la nne kwa mkwaju wa penati wakati Ghoulam Faouzi akiifungia Algeria tano pia kwa mkwaju wa penati ikiwa ni dakika ya 59.

Carl Medjani akafunga goli la sita dakika ya 72 huku Slimani Islam akipachika bao la saba dakika ya 75.

Farid Musa, Himid Mao Mkami, Kelvin Yondani, Haji Mwinyi Nadir Haroub na Aishi Manula walioneshwa kadi ya njano huku Mudathir Yahya akioneshwa kadi mbili za njano zilizopelekea kupata kadi nyekundu dakika ya 41 kipindi cha kwanza na kuiacha Stars ikicheza pungufu kwa muda wote uliosalia.



Comments