Mshambuliaji wa Barcelona, Neymar amempigia debe nyota mwenzake katika klabu hiyo, Lionel Messi akisema kuwa anastahili kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwaka huu 'Ballon d'Or'.
Kwa sasa Messi ndiye aliyepewa nafasi ya kutwaa tuzo hiyo baada ya msimu uliopita kuiwezesha Barcelona kutwaa mataji matatu kabla ya kucheza mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Copa America akiwa na Argentina.
Pia Neymar anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji watatu watakaochaguliwa kuwania tuzo hiyo itakayotolewa Januari, mwakani na huku kukiwa na matumaini kidogo ya kupewa anayeshikilia kwa sasa, Cristiano Ronaldo.
"Leo ndiye anayepewa nafasi. Na mwaka huu tuzo ya Ballon d'Or anastahili kukabidhiwa Messi ambaye ni mchezaji bora wa dunia na kila kitu kinachostahili anacho," Neymar aliliambia jarida la Mundo Deportivo.
"Natumaini nitafanya vizuri kwa kucheza sambamba na Messi. Ni mchezaji mzuri na chaguo langu," aliongeza staa huyo.
Comments
Post a Comment