MWAMBUSI KUTUA RASMI YANGA KUVAA VIATU VYA MKWASA



MWAMBUSI KUTUA RASMI YANGA KUVAA VIATU VYA MKWASA
Juma Mwambusi anatarajia kusaini mkataba wa kujiunga na              klabu ya Yanga

Juma Mwambusi anatarajia kusaini mkataba wa kujiunga na klabu ya Yanga

Kocha mkuu wa Mbeya City Juma Mwambusi ameshafikia makubaliano na uongozi wa Yanga ili kusaini mkataba wa kujiunga na klabu hiyo ambayo ni bingwa mtetezi wa ligi kuu Tanzania bara. Mwambusi anatarajiwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu kuchukua nafasi ya Charles Boniface Mkwasa aliyepewa jukumu la kuifundisha timu ya taifa 'Taifa Stars'.

Leo mchana Kocha Mkuu wa Mbeya City Fc, Juma Mwambusi, alikutana kwa dharula na mtendaji Mkuu wa klabu (Katibu Mkuu) kwa mazungumzo.
Pamoja na mambo mengine, katika mazungumzo hayo, Mwl Juma Mwambusi alitumia nafasi hiyo kuuaga rasmi uongozi ili kwenda kujiunga na timu ya Young Africans 'Yanga' ya Dar es Salaam.

Katika hali ya kawaida kabisa uongozi wa klabu umekubaliana na kile ambacho Mwl Mwambusi alikisema na kukiomba ikiwa ni kwa ajili ya manufaa ya klabu na manufaa yake kama kocha.
Klabu inachukua fursa hii kumshukuru Mwl. Juma Mwambusi kwa yote mazuri aliyofanya kwenye timu kwa kipindi chote cha miaka mitano ambacho amefanya kazi hapa kwa mafanikio makubwa.

Ikumbukwe kuwa Mwl Juma Mwambusi ni mmoja wa waanzilishi wa timu ya Mbeya City FC, hivyo uongozi unatambua na kuthamini mchango wake mkubwa ndani ya klabu tangu kuanzishwa mpaka hapa ilipofika.

Kwa niaba ya bodi, klabu, inamtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya ndani ya klabu ya Young Africans.
Kwa sasa benchi la ufundi la Mbeya City FC litabaki kuwa chini ya kocha msaidizi Meja Abdul Mingange(Rtd.) mpaka itakapotolewa taarifa nyingine.

Imetolewa na,
E.E.Kimbe
KATIBU MKUU
MCC FC



Comments