MKWASA, TAMBUA SIPO PEKE YANGU



MKWASA, TAMBUA SIPO PEKE YANGU
Kocha mkuu wa Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa

Kocha mkuu wa Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa

Na Nicasius N. Agwanda (Coutinho Suso)

Moja ya waandishi wazuri wa makala kwa ujumla wake (michezo na kwingineko), kaka yangu Ezekiel Kamwaga, aliweka bandiko katika ukurasa wake wa facebook akiwapongeza Taifa Stars kwa ujumla wa matokeo yake.

Lilikuwa bandiko fupi lakini aliloliandika kiufundi sana, akinukuu maneno ya mchezaji wa Madrid na Wales Gareth Bale kuwa  "It was a happiest defeat" ikiwa na maana ni kipigo cha furaha. 

Kikubwa alimaanisha juu ya ukomavu wa timu ya taifa na uwezo wake wa kupata wanachokihitaji hata wakiwa katika wakati ambao hawachezi vizuri huku pongezi zake zikienda kwa kocha Mkwasa. Alikuwa sahihi sana kwa tafsiri nzima aliyoitoa, hapa kwa lugha yetu tunasema mboni zake ni imara sana. 

Kwa jicho la kawaida ni rahisi sana kuwalaumu Taifa Stars kuliko kuwasifia, kwa jicho la kawaida ni rahisi kuona urahisi wa mipira aliyoshindwa kuiwahi John Bocco kuliko kujua majukumu mageni aliyopewa siku hiyo aliyatimiza kiasi gani na yalichangiaje yeye kuchoka vile pia hali ya uwanja ukilinganisha na kasi ya pasi za Samatta.

Haina maana kuwa ulihitaji kuwa malaika kulijua hili, hapana ila ulihitaji kujua walau ni kiasi gani Himid Mao ni muhimu kwa timu ya Taifa kwa sasa kuliko mtu mwingine yoyote. Usishangae, Maradona aliwahi kuamini kuwa Argentina ina Mascherano na wachezaji wengine 10 Katika kikosi cha kwanza na sio Messi.

Nazungumzia wale wachezaji ambao wanaweza kuweka uti wa mgongo, goti au shingo karibu kabisa na njumu ya mshambuliaji mwenye uchu, kuzuia shuti ambalo pengine lingepaa hawa wanaitwa Saviors (wakombozi). 

Lakini hapa nataka niende mbali zaidi, Taifa Stars kwa sasa ni zaidi ya inavyofikiriwa. Kisaikolojia unaweza kusema wameimarika kutokana na namna wanavyocheza pia pongezi kutokana na namna wanavyoukabili mchezo, kuanzia mechi ya Nigeria ungeliona hilo.

Hakuna mchezo ambao naamini upo akilini kwa Mkwasa kama ule unaofuata dhidi ya Algeria. Ndio ni timu bora sana kwa miaka ya karibuni, kizazi bora pia cha nchini kwao tangu miaka ya 80. Asilimia kubwa ya wachezaji wao wanacheza soka la kulipwa, mastaa wa nchi yao ni mastaa pia wa vilabu vyao. Lakini hiyo haifanyi mchezo kuwa umemalizika, wala haigeuzi soka kuwa riadha yaani mwenye kasi zaidi ndio atashinda. Mbinu za kuikabili Algeria  ndio kitu cha awali kabisa kwenye mchezo huu. 

Tahadhari ndio mbinu ya kwanza kabisa na sio woga. Hivi ni vitu viwili tofauti, underdogs wengi huingia mchezoni kucheza kwa woga na sio tahadhari. Ukicheza kwa woga unakaribisha mashambulizi kwako kupita maelezo na hii mara nyingi huwa kwa wachezaji na sio kocha.

Lakini hapa Mkwasa anatakiwa kuhubiri tahadhari kambini kwa Stars. Tucheze kwa uhuru huku tukiweka umakini kuwa Algeria wanaweza kupata matokeo muda wowote. Kujiamini kupita kiasi nalo ni tatizo.

Ieleweke kuwa asilimia 80 ya kikosi chao ni wachezaji wa kulipwa. Hii iliwaathiri South Africa chini ya Shakes Mashaba katika AFCON, walijiamini kupita kiasi, ingawa walitangulia kupata goli, ilihitaji nafasi tatu tu, Algeria kuongoza kwa magoli matatu na kumaliza mechi. Hivyo tahadhari ni jambo la kwanza kabisa. 

Sahau ya Malawi. Pamoja na imani kuwa Taifa Stars hucheza mechi kubwa vyema lakini uwezo dhidi ya Malawi hasa nyumbani inabidi utukune kichwa. Soka ni mchezo wa mwendelezo ama 'consistency'. Unaposhindwa kucheza vizuri kwa mfululizo inapelekea kuwa tabia yako.

Ni ngumu kuchukua chanya kutoka katika ule mchezo kwa jicho la kawaida hasa ukizingatia Algeria ndiye kitoweo unachotakiwa kukila mbeleni. Ukomavu kama alivyosema kaka yangu Kamwaga ni jambo jema lakini kuifunga Algeria ambayo kimsingi kulingana na viwango vya Fifa ndio namba moja kwa ubora Afrika, unatakiwa uwe katika kiwango bora cha udhaifu wako.

Maana yake ni kuwa unatakiwa kuitumia hali ya udogo kikamilifu kwa kucheza katika ubora wako unaowezekana (capitalize on your underdog syndrome). Hii ni pamoja na kutumia kila nafasi finyu utakayoipata. 

Katumbi karibu taifa. Sina maana ya kuwa tunahitaji kumleta Katumbi uwanjani la hasha. Hii ni kengele kwa wachezaji wetu bora Samata na Ulimwengu. Ile hali ya kuamua matokeo klabuni katika mechi kubwa inatakiwa kuhamia katika mechi kubwa kwenye jezi hizi za bluu.

Napendezwa na kiwango chao, hapana shaka katika hilo. Lakini katika soka kuna kitu kinaitwa 'Individual Brilliance' (uwezo binafsi). Hapa unategemea mchezaji wako bora atoke mafichoni kukubeba. Hiki ndicho tukisubiri kwa hamu. Hizi ni mechi ambazo wao watatizamwa sana na wapinzani, hivyo ni jukumu la kila mchezaji kuwalinda wachezaji bora (complementing your best players).

Ukiwafanya hawa wawe na hatari unaongeza kuhamaki (tension) kwa wapinzani hivyo kuongeza hatari yenu kwa ujumla. 

Mashabiki uwanja wa Taifa. Kuna jambo moja linakosekana tangu aondoke mzee wa kibrazil Maximo, nalo ni nguvu ya mashabiki. Algeria wanamiliki moja ya viwanja vyenye kutia woga sana, uwanja wa Stade 5 Juillet 1962, unaingiza mashabiki 85000, 25000 zaidi ya huu wa Benjamin Mkapa, haitokuwa rahisi kwetu kwa marudiano.

Unahitaji uwanja uwe na kelele za nyuki muda wote kuiweka Stars mahala salama, unahitaji kelele kumfanya Kapombe aendane na kasi na unyumbulifu wa Brahimi muda wote. Unahiatji kelele hizi kumpa nguvu Mwinyi asiye na uzoefu wa michezo mikubwa bado kummiliki Ryan Mahrez.

Mwisho wa siku unahitaji kelele hizi kuwaweka katika upweke Algeria kwa ujumla,unahitaji kelele hizi kumfanya Nyati Ulimwengu kuwekeza nyongeza ya nguvu yake katika mchezo huu. 

Kila kitu kinawezekana, goli 2 hazikuwa sahihi dhidi ya Malawi (tulihitaji na tungeweza zaidi) lakini inawezekana kwa Algeria. Mwimbaji wa zamani wa kundi la beatles John Lennnon aliwahi kukaririwa  "ukisema mimi naota, tambua sipo peke yangu, nina imani siku moja utaungana nasi, na siku hiyo ulimwengu utaishi na utakuwa kitu kimoja". Nami ninaamini hivyo, ipo siku ndoto itakuwa sahihi, na wengine wataungana nami baadae. MKWASA MAKE US DREAM, I'M NOT ALONE.

Ahsanteni, by Nicasius N Agwanda. (Coutinho Suso)

Instagram: @nicas.coutinho



Comments