Na David Nyembe, Mbeya
Mtanange wa ligi kuu Tanzania bara (VPL) baina ya miamba ya soka Simba SC dhidi ya Mbeya City umechukua sura mpya baada ya kocha wa Simba Dylan Kerr kukiri kwamba bado hajui nani atakayeanza.
Akizungumza na mtandao huu katika hafla fupi ya kusheherekea siku ya kuzaliwa kwa nyota wao Boniface Maganga, Kerr alibainisha kuwa kila mchezaji yupo tayari kuwavaa wenyeji wao huku akipata wakati mgumu wa nani atakayeanza.
"Hali ya hewa imekuwa nzuri hapa Mbeya, tumefanya mazoezi vizuri kila mchezaji yupo sawa. Ninapata wakati mgumu wa kuanzisha wachezaji kwani kila mmoja yupo kamili," alisema Kerr.
Kerr aliongeza kuwa ana deni kubwa kwa mashabiki wa Simba SC na timu kwa ujumla kwani wapo ugenini na kwamba watajitahidi kucheza vizuri katika umati mkubwa wa watazamaji watakaomiminika katika dimba la Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya baadaye hii leo.
Aidha Kerr aliwapongeza Hamis Kiiza na Boniface Maganga kwa kuwapatia keki ya kusheherekea siku za kuzaliwa kwao.
Pia Kerr aliweka bayana suala la Kiiza kuwa hakuna majeruhi katika timu hiyo na kwamba ataangalia amchezeshe au la.
Mitaa ya Jiji la Mbeya
Kumekuwa na ari na hamasa kwa kila mmoja huku wengi wakionekana na jezi za Mbeya City na Simba SC.
Aidha kumekuwa na maeneo mbalimbali ambayo yamening'inizwa jezi kuelekea mechi hiyo zikiuzwa kwa kati ya shilingi 12,000 hadi 20,000.
Hofu ya tunguli
Katika dimba la Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, katika kile kinachoonekana kuathiriwa na nguvu za ushirikina miongoni mwa mashabiki wa Mbeya City walianza kuulinda uwanja huo tangu jana hususani katika dimba la kuchezea ili kuzuia mianya ya kile kinachofahamika kama tunguli.
Baadhi yao walipoulizwa walisema hawaiamini kabisa Simba kwani inaweza kutupa vitu vyake ambavyo vitaiathiri Mbeya City ambayo itacheza kwa mara ya kwanza bila ya kuwa na Kocha Mkuu, Juma Mwambusi.
Comments
Post a Comment