KIPA TZ PRISONS: “TUTAIFUNGA STAND UNITED KWAO”


KIPA TZ PRISONS: "TUTAIFUNGA STAND UNITED KWAO"

Mohamed Yusuf 1

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam 

Baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 3-0 katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora, mlinda mlango namba moja wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Yusuph Mohamed amesema kuwa watahakikisha wanaifunga Stand United wikendi hii ili kuendelea kupanda juu ya msimamo wa ligi. 

Prisons ilinusurika kushuka daraja misimu miwili mfululizo iliyopita ipo katika nafasi ya tano ya msimamo ikiwa na alama 10 (pointi 5 nyuma ya vinara Yanga SC na Azam FC) imeshinda gemu 3 na kutoa sare mara moja. Chini ya kocha aliyeipa ubingwa wa Tusker Cup timu ya Mtibwa Sugar mwaka 2008 Salum Mayanga timu hiyo imeanza msimu huu kwa kasi. 

"Tunahitaji kuishinda Stand ili hesabu zetu ziendelee kuwa sawa. Kwenye msimamo tupo katika nafasi ambayo siwezi kusema ni mbaya, ila tunahitaji kusogea juu zaidi. Tumekuwa tukicheza kwa nidhamu, nguvu na maarifa kuhakikisha hatuingii katika nafasi mbaya kama misimu iliyopita", alisema Yusuph wakati alipozungumza na mtandao huu. 

Prisons tayari imefanikiwa kufunga jumla ya magoli sita na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tano inawategemea zaidi washambuaji wao Jeremiah Juma na Ally Manzi ambao kila mmoja amekwishatupia kambani mara mbili katika gemu 6 zilizopita. Wapo nyuma ya Simba na Mtibwa Sugar kwa tofauti ya pointi mbili tu.



Comments