GIANLUIGI DONNARUMMA ANAWAKUMBUSHA AC MILAN WAPI WALIPOTOKA.


GIANLUIGI DONNARUMMA ANAWAKUMBUSHA AC MILAN WAPI WALIPOTOKA.

gianluigi donnarumma

Mwanadamu husifiwa kwa vitu vingi sana katika maisha yake.Miongoni mwa sifa ambazo mwanadamu huweza kupewa ni kitendo cha kuwa na maamuzi sahihi kwa wakati sahihi.

Nasema hivyo kwa kumpongeza Kocha wa sasa wa AC Milan Sinisa Mihajlovic kwa maamuzi yake yake muhimu ya kumpa nafasi golikipa kijana wa AC Milan Gianluigi Donnarumma kucheza mchezo wa serie A akiwa na umri wa miaka 16 tu dhidi ya Sassuolo.

Inawezekana uamuzi wa kocha Sinisa ukatafsiriwa kwa namna tofauti na watu wengi lakini kwangu ni uamuzi ambao umewanyooshea kidole watendaji wa klabuya Ac Milan hasa mmiliki Silvio Berlusconi na makamu wake Adriano Galliani.

Labda niwakumbushe tu kuwa Gianluigi Donnarumma ni kipa ambaye ametokea katika timu ya vijana ya Ac Milan.Kocha Sinisa Mihajlovic ameamua kumpa nafasi Donnarruma baada ya kutoridhishwa na uwezo wa kipa namba moja wa timu hiyo Diego Lopez.

Anachofanya Mihajlovic ni kuwakumbusha mabosi wa Ac Milan umuhimu wa kuwekeza katika timu za vijana za klabu hiyo ili kupata wachezaji wazuri watakao isaidia Ac Milan siku za usoni.Miaka ya nyuma klabu ya AC Milan ilisifika sana kwa kuzalisha wachezaji vijana wenye vipaji vikubwa ambao walikuja kuwa msaada mkubwa katika klabu hiyo.

Mfano wa wachezaji hao ni Paolo Maldini.Maldini ni miongoni mwa wachezaji wachache waliokulia katika timu za vijana za Ac Milan na zaidi Maldini amestaafia Ac Milan akicheza jumla ya michezo 647 kuanzia mwaka 1985 mpaka mwaka 2009.

Si Maldini peke yake,yupo nyota mwingine aliyekulia katika klabu ya Ac Milan ambaye alitamba kwa uwezo wake ndani ya uwanja hasa katika eneo la ulinzi wa kati.

Wengi walipenda kumwita 'Sweeper' ikimaanisha mtu wa mwisho katika idara ya ulinzi ambaye alikuwa na jukumu la kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani lakini pia kuokoa mipira yote hatari inayoelekea golini.
Huyu si mwingine bali ni Franco Baresi

Si hao wawili tu wapo wengine ambao wamepitia katika mifumo ya kutengeneza vijana ya Ac Milan kama Alessandro Costacurta ,Cristiano Brocchi,Demetrio Albertini,Francesco Antonioli ,Mauro Tassotina wengine wengi .

Utaratibu wa kuzalisha vijana katika klabu ya Ac Milan ulianza kufifia pale waziri Mkuu wa zamani wa Italia Silvio Berlusconi alipoichukua timu hiyo mwaka 1986.
Berlusconi alikuja na sera tofauti kabisa na iliyokuwepo awali.Yeye aliamini katika kununua mastaa mbalimbali ili waje kuipa Ac Milan mafanikio.

Milan ilianza kuonekana tofauti kwa kuwanunua wachezaji nyota wakati huo kama Ruud Gullit,Marco Van Basten,Frank Rijkaad,Marcel Desailly,Andry Shevchenko,Filipo Inzaghi,Oliver Bieroff,Manuel Rui Costa,Alessandro Nesta na wengineo wengi.

Sera yake hiyo ilionekana kuwa nzuri na yenye mafanikio kwani katika kipindi cha muda mfupi tu Ac Milan ilitwaa mataji mengi sana ya ndani na nje hasa michuano ya Ulaya.Lakini sera hii haikuwa rafiki kwa mfumo wa vijana wa timu ya Ac Milan kwani nyota wengi waliozalishwa katika klabu hiyo waliondoka katika klabu hiyo na kujiunga na vilabu vingine.

Baadhi ya nyota walikokulia katika timu za vijana za Ac Milan lakini wakaondoka hasa mwishoni mwa miaka ya 90 ni pamoja na Pierre Emerick Aubameyang ambaye anaichezea klabu ya Borussia Dortmund,Alessandro Matri yupo Lazio,Fabrizio Miccoli na wengineo wengi.

Hapa ndipo AC Milan ilipopoteza alama yake kwani mpaka sasa klabu hiyo ina wachezaji wachache sana ambao wamekulia katika mfumo wa vijana wa klabu hiyo.
Kikosi cha kwanza cha Ac Milan kwa sasa kina wachezaji wanne tu ambao wamekulia katika timu za vijana za Ac Milan.Wachezaji hao ni Ignazio

Abate,Mattia De Sciglio,beki wa kulia wa timu hiyo David Calabria na kipa wa sasa Gianluigi Donarruma.

Inawezekana miaka ya karibuni wachezaji wanaotoka katika timu za vijana za Ac Milan wakawa hawana ubora unaohitajika katika klabu lakini wanapaswa kupewa nafasi kama ambavyo kocha Sinisa Mihajlovic alivyomp nafasi Gianluigi Donnarumma.

Wapo wachezaji kama Hachim Mastour ambate yupo kwa mkopo Malaga,Andrea Petagna yupo kwa mkopo Ascoli ,Simone Verdi yupo Eibar kwa mkopo hawa wote wamekulia katika timu za vijana za Ac Milan na wanaweza kuisaidia timu hiyo endapo watapewa nafasi.

Natumai Gianluigi Donnarumma ataendelea kuisadia Ac Milan na kuwakumbusha viongozi wa klabu ya Ac Milan kuwekeza zaidi kwa vijana.



Comments