Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Huu ni msimu wa pili katika ligi kuu Tanzania bara kwa klabu ya Stand United ya Shinyanga. Timu hii ilianzishwa rasmi mwaka 2012 na ikafanikiwa kucheza ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2014/15 msimu ambao walipambana hadi dakika ya mwisho kuhakikisha wanasalia katika ligi.
Msimu huu, Stand imekuwa moja ya timu zenye udhamini mkubwa (ukiachana na ule wa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, Vodacom Tanzania na AzamTv), pia imewasaini wachezaji wengi wenye majina makubwa na washindi wa ligi hiyo. Hamak Ndikumana Kakut ni straika raia wa Rwanda, Elius Maguli, Amri Kiemba, Nassor Masoud 'Cholo', Hassan Dilunga, Jacob Masawe ni baadhi ya wachezaji wapya katika timu hiyo.
Mfaransa, Patrick Liewig ndiye kocha mkuu wa timu hiyo. Liewig ni mwalimu ambaye amewahi kuifundisha Simba SC msimu wa 2012/13 kwa miezi 6 ameisaidia timu hiyo kushinda michezo mitatu ( 3) kati ya sita ( 6) msimu huu na hivyo kukusanya alama 9 sawa na Toto Africans ya Mwanza. Stand ipo nafasi ya 7 ya msimamo itacheza na Tanzania Prisons Jumamosi hii katika uwanja wa Kambarage.
Awali ilipoteza michezo miwili kati ya mitatu ya mwanzo katika uwanja wao wa nyumbani. Walifungwa na Mtibwa Sugar katika gemu ya ufunguzi, wakapoteza tena mbele ya Azam FC kabla ya kupata ushindi wa kwanza katika raundi ya Tatu dhidi ya African Sports. Wakaishinda JKT Ruvu katika uwanja wa Karume, Dar es Salaam, kisha wakapoteza dhidi ya Simba SC.
Stand iliifunga Mbeya City katika gemu ya mwisho kabla ya ligi kusimama kupisha michezo ya kimataifa. Kimatokeo naweza kusema kuwa Liewig bado anaendelea kufanya vizuri. Akiwa na timu mpya yenye wachezaji wengi wageni, kuashinda gemu 3 kati ya 6 si matokeo ambayo yanaweza kuwafanya viongozi, mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kulalamika.
Nawashangaa viongozi wa klabu hiyo kukimbilia katika vyombo vya habari na kumsema vibaya kocha wao eti ni mtu ambaye hataki ushahuri!. Ndiyo mtu asiyekubali ushahuri si rahisi kufanikiwa ila si kweli kwamba kila wanachotaka watawala wa timu hiyo kitakubali na kocha. Wakati mwingine inapaswa kuwaacha huru makocha wafanye kazi zao vile wanavyotaka. Kinachoendelea Stad ni kitu sahihi.
Kama kuna matatizo mahali wanapaswa kukaa wenyewe ndani ya timu na kumaliza tofauti hizo, kukimbilia katika vyombo vya habari ni sawa na kuchochea presha isiyo na sababu kwa benchi la ufundi kwa kuwa timu itakapofanya vibaya mashabiki watasema 'sababu ya kocha wao kushindwa kuwasikiliza'. Stand wanajiweka katika daraja la timu za juu lakini si kweli wanapaswa kuendelea kuwa wavumilivu ili wafanikiwe kuwa na timu imara ya muda mrefu.
Liewig ni kocha nayeeleweka kwa wachezaji, nafikiri hata baadhi ya matokeo mabaya waliyopata msimu huu yatakuwa yanaanzia katika uongozi wa juu na si kwa kocha. Kitu muhimu kwa viongozi wa Stand ni kutambua kuwa kocha ndiye hupendekeza kambi ya timu iwe wapi, kwa muda gani na kazi ya utawala ni kutekeleza mahitaji muhimu, ushahuri uwe mzuri na usiwe wa kumlazimisha kocha.
Alama 9 katika gemu 6 ni matokeo mazuri sana kwa timu changa kama Stand, ukizingatia tayari wamecheza na Mtibwa, Azam FC, Simba na Mbeya City. Liewig aachwe afanye kazi yake viongozi wa Stand United wasimtengenezee ubaya ambao hana.
Comments
Post a Comment