Cesc Fabregas na Robin Van Persie wiki hii wamejiunga na kundi la wachezaji waliotimiza idadi ya mechi 100 katika timu zao za taifa.
Wakati Van Persie alitimiza mechi yake ya 100 akitokea benchi katika mchezo dhidi Kazakhstan, Fabregas aliifikia rekodi hiyo akiwa na kitambaa cha unahodha wa Spain katika mchezo wa Jumatatu dhidi ya Ukraine.
Wawili hawa wamekuwa ni watu muhimu sana katika vikosi vya timu zao kwa miaka kadhaa na sasa wanajiunga na listi ya kipekee ya mastaa na hata wasiokuwa na majina makubwa ambao wamefikia idadi ya mechi 100 za kimataifa.
Hata hivyo, wawili hao itawabidi wacheze zaidi katika muongo unaokuja kutoka sasa, ili waweze kufikia rekodi ya Ahmed Hassan, mwanasoka ambaye amecheza mechi nyingi za kimataifa kuliko mwanasoka yeyote duniani-akiichezea Misri mechi 184.
Sasa akiwa na miaka 40, mwanasoka wa zamani wa Besiktas na Anderlecht alianza kuicheza Misri mnamo mwaka 1995 kabla ya kumaliza utumishi katika timu ya taifa mwaka 2012. Hiyo misimu 10 ya kimataifa.
Huku kukiwa na ongezeko la mechi za kirafiki, kufuzu, na michuano rasmi, sio jambo la kushangaza kuona wachezaji wengi wakiwemo kwenye listi hii.
Golikipa Iker Casillas yupo katika nafasi ya 8 katika listi hii akiwa kaitumikia Spain katika mechi 164 wakati golikipa wa Italia Ginaluigi Buffon akiwa hayupo nyuma sana ana mechi 151.
Miongoni mwa mataifa makubwa 20 yenye mafanikio zaidi, wachezaji 16 wamecheza zaidi ya mechi 100 katika timu ya taifa ya Marekani-kiungo wa zamani wa Coventry City Cobi Jones akiichezea mechi 164, mechi 7 zaidi ya Gwiji wa soka wa USA London Donovan.
Ma-giants wa America ya Kusini Brazil na Argentina wana wachezaji 9 katika listi hiyo. Claudio Taffarel, Cafu, Lucio na Roberto Carlos-wanaume waliokuwa wanaunda ukuta wa kikosi cha Samba wote wameichezea Brazil mechi 100. Javier Zanetti, anaiongoza listi ya Argentina kwa kuichezea mechi 147 – miaka 17 ya kuitumikia timu yake ya taifa. Staa wa sasa wa Argentina Lionel Messi itabidi awavuke Diego Simeone, Roberto Ayala na Javier Mascherano kabla ya kuanza kufikiria rekodi ya Zanetti.
Ujerumani ina wachezaji 11 waliocheza mechi zaidi ya 100. Miroslave Klose, mfungaji bora wa muda wote wa kombe la dunia, ameichezea Ujerumani mechi 137 wakati Lothar Matthaus akiichezea mechi 150.
Washindi wa kombe la dunia wa Spain Xavi, Andres Iniesta, Sergio Ramos, Xabi Alonso, Carles Puyol na Fernando Torres wote kwenye listi hiyo.
Wachezaji zaidi ya sita wamecheza mechi zaidi ya 100 katika timu ya taifa ya Ufaransa na wote walihusika katika kikosi cha Les Bleus kilichoshinda ubingwa wa dunia wa mwaka 1998.
Mlinzi Lilian Thuram amecheza mechi 142, wakati Zinedine Zidane, Thierry Henry, Marcel Desailly, Didier Deschamps na Patrick Vieira wote wamefikia rekodi ya mechi 100.
Katika mataifa yanayounda Great Britain-England inaongoza kwa kutoa wachezaji wengi kwenye listi-wachezaji 9, akiwemo David Beckham, Bobby Moore na Wayne Rooney-lakini cha kushangaza ni kwamba Wales haijawa na mchezaji aliyetimiza mechi 100.
Mchezaji wa zamani wa Everton Neville Southall anaongoza kwa kucheza mechi 92 huku Ryan Giggs, pamoja na kutajwa kuwa mwanasoka bora kabisa wa nchi hiyo akiwa amecheza mechi 64-na inawezekana idadi hii imetokana na nchi kushindwa kucheza kwenye michuano mikubwa katika wakati wake.
Robbie Keane, John O'Shea na Shay Given-wote wakiwa na miaka 33, wanaendelea kuitumikia Ireland ya Martin O'Neill wakati Steve Staunton na Kelvin Kilbane, wakikamilisha listi ya wachezaji wa nchi hiyo waliocheza mechi zaidi ya 100.
Kenny Dalglish ni mscotland pekee ambaye amecheza mechi zaidi ya 100.
Comments
Post a Comment