Nahodha wa timu ya Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' amekiri kuwa, anamuogopa golikipa wa Azam FC pale linapokuja suala upigaji penati dhidi ya golikipa huyo.
Manula alipangua mkwaju wa penati uliopigwa na Thabani Kamusoko wakati wa mchezo kati ya Yanga dhidi ya Azam uliopigwa kwenye uwanja wa taifa. Mkwaju huo wa penati ulikuwa ni wa kuamua matokeo ya mchezo huo lakini Manula akaisaidia timu yake kulazimisha matokeo ya sare ya kufungana kwa goli 1-1 dhidi ya Yanga.
"Aishi Manula ni kipa mzuri namheshimu sana, hata tukiwa kwenye timu ya taifa ni kipa mzuri kwenye penati, hata mimi namuogopa, japo ni jambo la kawaida kukosa penati", Cannavaro alikiri wakati akizungumza na mtandao huu baada ya mchezo huo kumalizika.
"Tumetengeneza nafasi nyingi sana, hata hiyo penati tusingeipata kama tungekuwa hatutengenezi nafasi. Azam wamecheza vizuri hasa kipindi cha pili ndio maana wakaweza kusawazisha goli".
"Yanga tupo kwenye ubora wetu, bado tunaongoza ligi na tunaimani mechi ya Jumatano tutafanya vizuri, matokeo ya mechi hii yatatupa morali ya kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi zijazo".
Juhudi za kumpata Manula ziligonga mwamba baada ya wachezaji wa Azam kuonekana kuchukizwa na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo kwani baada ya mchezo kumalizika wengi wao walikimbia kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Comments
Post a Comment