BARCELONA, REAL MADRID, BAYERN ZAFANYA KUFURU TUZO YA MWANASOKA BORA DUNIANI (Ballon d'Or) ...MAN CITY YAJIKAKAMUA, ARSENAL, CHELSEA ZAAMBULIA NAFASI MOJA, MAN UNITED YATOKA MIKONO MITUPU
Winga wa Wales Gareth Bale ndiye mchezaji pekee kutoka Uingereza aliyejumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 23 watakaowania tuzo ya mwanazoka bora duniani - Ballon d'Or, akiwa ameingia kwenye orodha hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Bale ni miongoni mwa wachezaji 11 kutoka ligi kuu ya Hispania (La Liga) wanaowania tuzo hiyo huku Premier League na Bundesliga zikiwa zimetoa wachezaji watano kila moja.
Manchester City ya England imeingiza wachezaji watatu Sergio Aguero, Kevin De Bruyne na Yaya Toure huku Chelsea ikiambulia mchezaji mmoja Eden Hazard.
Arsenal pia imefanikiwa kupata nafasi moja kupitia kwa Alexis Sanchez wakati Manchester United, Liverpool na vilabu vingine vya England vikitoka patupu.
Kwa mara nyingine tena Real Madrid na Barcelona zimetawala kwenye orodha hiyo itakayotoa mchezaji bora wa dunia Januari 11, 2016 huko Zurich.
Bale anaungana na mshindi wa mwaka 2014 Cristiano Ronaldo, Karim Benzema, Toni Kroos na James Rodriguez katika jumla ya wachezaji watano wa Real Madrid walioingia kwenye orodha ya Ballon d'Or, wakati Lionel Messi akiwa na Neymar, Luis Suarez, Javier Mascherano, Andres Iniesta na Ivan Rakitic kwa upande wa Barcelona yenye wachezaji sita.
Bayern Munich nayo imeingiza wakali watano Robert Lewandowski, Thomas Muller, Manuel Neuer, Arjen Robben na Arturo Vidal, huku Paul Pogba wa Juventus na Zlatan Ibrahimovic wa Paris Saint-Germain wakikamilisha orodha hiyo.
Arsene Wenger na Jose Mourinho ni miongoni mwa makocha 10 wanaowania tuzo ya kocha bora wa mwaka sambamba na Luis Enrique wa Barcelona na Pep Guardiola wa Bayern Munich.
Makocha wengine ni Massimiliano Allegri wa Juventus, Unai Emery wa Sevilla, Laurent Blanc wa PSG, Diego Simeone wa Atletico Madrid na Carlo Ancelotti aliyetimuliwa Real Madrid kiangazi kilichopita, wakati kocha wa Chile Jorge Sampaoli naye ameingia kwenye orodha hiyo.
Mshambuliaji wa Real Madrid Gareth Bale (kulia) ni Mwingereza pekee kwenye orodha ya wachezji wanaowania Ballon d'Or
Cristiano Ronaldo (kushoto) mchezaji mwingine wa Real Madrid katika orodha ya wanasoka 23 wanaowania Ballon d'Or
Mastaa wa BarcelonaLionel Messi na Neymar nao wamo
Mshambuliaji wa Manchester City Sergio Aguero ni mmoja wa wachezaji watano wa Premier League waliojumuishwa kwenye list ya Ballon d'Or
Alexis Sanchez wa Arsenal (katikati) nyota mwingine wa Premier Legue kwenye kimbembe cha Ballon d'Or
Kocha wa Chelsea Jose Mourinho anawania nafasi ya Kocha bora wa mwaka duniani
Kocha wa soka la wanawake wa England Mark Sampson anatajwa miongoni mwa makocha wanaowania nafasi ya kocha bora wa soka la wanawake
Comments
Post a Comment