ACHANA NA SOKA, HAYA NDIO MAISHA YA ABDI KASSIM NJE YA UWANJA…


ACHANA NA SOKA, HAYA NDIO MAISHA YA ABDI KASSIM NJE YA UWANJA…
Abdi Kassim 'Babbi' (anaemiliki mpira) akiwa anakipiga              kwenye timu yake ya UiTM FC nchini Malaysia

Abdi Kassim 'Babbi' (anaemiliki mpira) akiwa anakipiga kwenye timu yake ya UiTM FC nchini Malaysia

Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam

Mwanasoka wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Kassim 'Babbi', 31, yuko likizo na mkewe Mariam Abdulkadir Kheri nchini Malasyia ambako Babbi amekuwa akicheza mpira wa kulipwa kwa miaka miwili sasa.

Babbi amemaliza mkataba wake wa awali na klabu ya UITM FC ameuambia mtandao huu kuwa, muda wowote anaweza kusaini mkataba kwa kuwa kuna klabu tatu hadi nne zinamuhitaji ila kwa sasa yuko kwanza likizo na 'mama watoto wake'.

Mtandao huu umefanya mahojiano na mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Mtibwa Sugar, Yanga SC, Miembeni FC na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambaye anafunguka kuhusu mambo ya nje ya uwanja (hususani familia yake).

Mchezaji huyu mwenye kupiga mashuti ya mbali amefanikiwa kupata watoto watatu, mtoto wa kwanza ana umri wa miaka saba na watoto wawili 'mapacha' wana miaka mitano.

"Maisha yetu kiujumla tunaishi Zanzibar ila kwa sasa nipo na mke wangu Malasyia. Watoto wapo Zanzibar wakiendelea na masomo", anasema Abdi kuhusu familia yake yenye watu watano.

Abdi alimuoa Bi. Mariam takribani miaka minne iliyopita anasema kuwa ameamua kukaa mbali na watoto wake kwa kuwa anahitaji muda zaidi wa kufanya kazi yake akiwa 'huru'.

"Ili nicheze vizuri uwanjani nahitaji muda wa kupumzika, kuna uwezekano wa wanangu kuja huku (Malasyia) kuendelea na masomo lakini nimetaka kuwa 'free' na kazi yangu na kupumzika vizuri ili 'nipa-form' vizuri katika game. Kitu cha msingi ni kuitazama kwa karibu familia wakiwa nyumbani (Zanzibar). Nimekuwa nikiwatumia ada ya shule, bila shaka nitarudi kuwaona".  

Kuhusu maisha ya Malasyia, Babbi anaaema; " Nimeshayazoa, mke wangu pia anafurahia maisha ya huku. Tunaishi vizuri, hali ya hewa si tatizo yani ni mazuri sana".

Ni chakula gani ambacho Babbi anakipendelea kula akiwa na familia yake?

"Nikiwa na familia napendelea sana 'kifungua kinywa-break fast' chai ya maziwa, chapati na matunda, mchana napendelea kula wali na 'samaki wa, usiku tunakula matunda tu au urojo".

Babbi ni tofauti sana na wachezaji wengi kwani hapendelei muziki ila na anasisitiza kuwa hakuna mwanamuziki yeyote anayemvutia katika dunia hii, ni mtu ambaye anahusudu sana sanaa ya vichekesho.

"Napenda sana filamu za vichekesho 'comedy' kwa kuwa napenda kuwa na furaha kila wakati. Navutiwa sana na mchekeshaji wa Zanzibar, Halikuniki".



Comments