Tanzania itakuwa mwenyeji wa kozi ya waamuzi chipukizi barani Afrika ambao bado hawajapata beji za FIFA, kozi hiyo itakuwa ya siku nne kuanzia kesho Septemba 26 hadi 30. Itakuwa na jumla ya washiriki 29 kutoka kwenye nchi za Afrika huku Tanzania ikiwakilishwa na waamuzi wawili.
Abdalla Kambuzi kutoka Shinyanga na Shomari Lawi kutoka Kigoma ni waamuzi wawili pekee watakaoiwakilisha Tanzania kwenye kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi wa FIFA kutoka Afrika Kusini, Mauritius, Malawi na Misri.
Kozi hiyo itafanyikia kwenye ukumbi wa Holliday Inn Hotel na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeshukuru kuwa mwenyeji wa kozi hiyo huku likiamini fursa hiyo waliyoipata wamuuzi wa Tanzania itawasaidia kupanda viwango na baadae kufika kwenye hadhi ya beji ya FIFA.
Afisa habari wa TFF Baraka Kizuguto amefafanua kuwa, waamuzi chipukizi haimaanishi kwamba waamuzi hao ni wadogo kiumri lakini badala yake ni wageni au chipukizi kwenye fani hiyo ya uamuzi wa mchezo wa soka.
"Mwamuzi anaweza akawa na umri wa miaka 30 na kuendelea, lakini akawa amechelewa kuingia kwenye fani ya uamuzi hivyo mwamuzi huyo atatambulika kama mwamuzi chipukizi", amefafanua Kizuguto.
Comments
Post a Comment