SIMBA NA YANGA ZASISITIZA HAZITAKUBALI KUCHEZA SAA 9 MCHANA ILI KUPISHA LIGI YA HISPANIA


SIMBA NA YANGA ZASISITIZA HAZITAKUBALI KUCHEZA SAA 9 MCHANA ILI KUPISHA LIGI YA HISPANIA

KLABU za Yanga na Simba zimesema, hazitakubali kucheza mechi zao za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara 'mchana', kama ambavyo wadhamini washiriki wa Ligi hiyo, Azam Media wanavyoshawishi.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam zimesema kuwa, wadhamini hao wapo katika mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) wakitaka mechi za Ligi hiyo sasa zifanyike kuanzia saa 9:00 mchana ili kutoa nafasi ya kuonyesha 'live' na baadae kituo hicho kuonyesha michezo mingine ya Ligi ya Hispania.
Akizungumza jijini Dar es Salam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema kuwa, Klabu yake haitakubali kucheza mechi mchana kwasababu itaathiri katika kupata mapato.
Manara alisema kuwa, mbali na suala la mapato, pia kiufundi, kucheza mchana kutawaumiza wachezaji wao kutokana na hali ya hewa ya jua iliyopo Dar es Salaam tofauti na wanavyotaka kulinganisha na baadhi ya mechi za Ulaya zinazochezwa mchana.
"Klabu ya Simba tunasema hatuko tayari kucheza mechi yoyote mchana, tunashukuru kiasi wanachotupa Azam lakini haiwezi kutuumiza kwa kubadili muda wa kuanza kwa mchezo, sisi sehemu kubwa ya fedha tunazotegemea ni za mapato ya milango," alisema Manara.
Manara alisema, mechi zitakapochezwa mchana zitawaathiri kiuchumi na kiufundi, kwasababu itabidi timu za vijana zichezwe saa 5:00 asubuhi na kuwapa chakula cha mchana saa 4:00 asubuhi.
Kiongozi huyo aliwatahadharisha viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi kulikataa pendekezo hilo, kwasababu itawafanya wachezaji kuathiri viwango kutokana na hali ya jua la Dar es Salaam linavyochoma.
Naye, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha alisema kuwa, ni vema kila jambo kabla ya kufikia maamuzi, viongozi waahusishe wadau wao ambao ni Klabu zinazoshiriki Ligi hiyo.
Alisema kuwa, kwa kufanya mazungumzo na kila upande na kufikia makubaliano, Ligi itachezwa kwa ufanisi na kila upande utajiandaa na mazingira husika.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Baraka Kizunguto alisema kuwa, ni kweli kuna baadhi ya mechi zinazohusisha Klabu hizo zitakazochezwa mchana na kuitaja mojawapo kuwa ni kati ya Yanga na Mgambo JKT.
Azam Media iliingia mkataba wa miaka mitatu na TFF, kwa ajili ya kuidhamini Ligi hiyo, wenye thamani ya sh. 5.56 Bil, wakati wadhamini wakuu, Kampuni ya Vodacom mwaka huu walisaini mkataba mwingine wa miaka mitatu wenye thamani ya sh. 6.9 Bil.
Hata hivyo, Simba na Yanga pia wanadhaminiwa na bia ya Kilimanjaro, wakati benki ya NMB inaidhamini timu ya Azam.





Comments