Baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Yanga dhidi ya JKT Ruvu, mtandao huu ulimfuata beki na nahodha wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' kutaka kujua nini siri ya mafanikio ya timu yake kupata ushindi wa kila mechi ambazo wamecheza hadi sasa huku wakiwa wamefunga magoli tisa na wao kuruhusu goli moja tu.
"Sisi sasahivi tumebadilisha mfumo, tunachezea sana mpira nadhani hata tukifika eneo la goli tunatakiwa kutulia kwa ajili ya kufanya maamuzi mazuri tunapokuwa kwenye eneo la hatari.", alisema Cannavaro huku akionekana kujiamini kwa kiasi kikubwa kwa kile anachokisema.
Kuhusiana na kucheza mechi tatu bila kupoteza huku safu yake ya ulinzi anayoiongoza ikiwa imeruhusu goli moja pekee, Cannavaro amesema haoni kama ni vibaya wao kufungwa goli moja kwenye mechi tatu huku akilisifia goli ambalo wamefungwa na JKT Ruvu.
"Goli walilotufunga JKT Ruvu ni goli zuri kwasababu walipata faulo wakapiga, mpira ukatugonga tukachelewa kwenda 'kublock' wakapiga wakapata goli, ni goli zuri sio baya lakini bado sio mbaya kwetu sisi kufungwa goli moja kwenye mechi tatu tulizocheza".
"Sio mbaya sisi kucheza mechi tatu na kufungwa goli moja nahii inatokana na kucheza na timu ngumu lakini bado sio mbaya kwa upande wa 'defense' kuruhusu goli moja kwenye mechi tatu".
Kuelekea mchezo wao dhidi ya Simba Cannavaro amesema Simba ni timu kama timu nyingine ambazo wamechea nazo na wao wamejipanga kuchomoza na ushindi kwenye kila mechi wanayocheza na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mechi dhidi ya Simba ili kuishangilia timu yao.
"Simba ni timu ya kawaida kama timu timu nyingine ambazo tumekutana nazo, kwa upande wetu sisi tumejipanga kushinda kila mchezo na nawaomba tu wapenzi wa Yanga wajitokeze kwa wingi waje waishangilie timu yao kwasababu mchezo utakuwa ni wakawaida tu".
"Kauli mbiu yetu ni kwamba, kila mechi tunayocheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani tunatakiwa tushinde si chini ya goli mbili na kuendelea".
Comments
Post a Comment