SARE YA CHELSEA YAZIDI KUMWEKA MATATANI STEVE MCCLAREN NEWCASTLE



SARE YA CHELSEA YAZIDI KUMWEKA MATATANI STEVE MCCLAREN NEWCASTLE

Kuongoza kwa 2-0 hadi dakika 10 za mwisho na kisha kuruhusu Chelsea izawazishe na kutoa sare ya 2-2, kumewakwaza mashabiki wa Newcastle huku kocha Steve McClaren akizidi kukalia kuti kavu kutokana na matokeo mabovu ya mfululizo.

Katika mchezo huo wa Premier League, Newcastle inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani, ilionekana kama itaokota ushindi wake wa kwanza lakini magoli ya Remires na Willian yakazima njozi zao.

Kuna kila dalili za McClaren wa Newcastle United kufungashiwa virago endapo hatopambana vya kutosha hii ikiwa pia ni baada ya kutolewa katika michuano ya Kombe la Ligi (Capital One).

Newcastle ilibamizwa na Sheffield Wednesday kwa bao 1-0 hivyo kuzua wasiwasi wa kocha huyo kuendelea kuishikilia nafasi hiyo.

Aidha Magpies wamepoteza mechi nne mfululizo wakishinda moja tu dhidi ya timu ya daraja la pili, Northampton.

McClaren alikaririwa akisema "Kazi imekuwa ngumu tofauti na nilivyofikiri, na watu wanasema kuna mgogoro unatunyemelea, ni kweli kwani tunastahili kulaumiwa," alisema kocha huyo.

Kwa mwaka huu (nusu ya msimu uliopita hadi msimu huu), Newcastle imeshinda mechi nne za EPL kwa mara ya mwisho ilikuwa Januari 31 ilipowazabua Hull City mabao 3-0.


Comments