Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Sunday Oliseh alikiri kuwa na hofu ya kupoteza pambano lake la kwanza kama mwalimu wa timu ya Taifa ya Nigeria 'Super Eagles' na nahodha wake, Ahmed Musa alinukuliwa akisema ' hakuna timu ndogo katika soka la kisasa', mwisho nilipenda kauli nzuri ya 'staa wa mechi' Mbwana Samatta aliposema 'Mwalimu Mkwassa anaeleweka sana kwa wachezaji, apewe muda zaidi'.
Hakika kila mtu anazungumza lake kuhusu mchezo wa Jumamosi iliyopita baina ya timu ya Taifa ya Tanzania ' Taifa Stars' na Nigeria. Je, Matokeo yametenda haki?. Watanzania wengi nwamefurahishwa na kiwango cha timu yao kiujumla. Kwa maana ya ilivyocheza na ilipotoka kabla ya kuwavaa Nigeria.
Upande wangu pia naungana na walio wengi juu ya kiwango cha wachezaji wa Stars lakini, katika upande wa matokeo hapana. Stars ilipaswa kuishinda ' Super Eagles' katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kupata alama tatu za kwanza katika kundi. Alama moja ni nyingi pia hasa katika michuano yenye gumu sita kwa kila timu.
Nafasi ambazo alipoteza kiungo mshambulizi, Mrisho Ngassa hazikupatikana upande wa wapinzani wao kwa kuwa Stars ilichezaji kwa umakini na nidhamu ya hali ya juu katika kujilinda. Matokeo hayajatenda haki kwa upande wa Stars kwa kuwa Ngassa alishindwa kuwa mtulivu na kutumia vizuri nafasi mbili za wazi.
KWANINI MKWASSA ANAITWA 'MASTER'…
Kitendo cha kuwaanzisha vijana chipukizi, Farid Musa katika wing ya kushoto, Mudathir Yahya na Himid Mao kama viungo wa kati ilikuwa ni 'mshangao' hata upande wangu, nikiri. Nilikuwa na hakika kuhusu kuanza kwa Himid lakini hadi katika ufanyaji wa 'sub' Mkwasa aliendelea kuwashangaza watu. Alijiamini katika kila kitu, kuanzia mfumo wake, upangaji wa timu, usomaji wa mchezo na alishikilia tumaini moja tu 'kuishinda Nigeria'.
Tatizo pekee ambalo anaweza kukutana nalo katika siku za mbele ni muendelezo wa viwango vya wachezaji wake watakaporudi katika ligi kuu Tanzania bara inayotaraji kuanza Jumamosi hii, lakini kiujumla ni mwalimu pekee ambaye hajashambuliwa kwa itikadi za klabu kuanzia katika uteuzi wake wa wachezaji wa timu ya Taifa hadi katika upangaji wake wa timu.
'Vichwa Vitatu' vilivyokuwa katika benchi la ufundi (Mkwasa, msaidizi wake, Hemed Morocco na mshahuri mkuu wa timu Abdallah 'King Mputa' Kibadeni) walikuwa katika ubora, umakini wa kufikiri na kufikia maamuzi.
Mkwasa alitaka timu yake ishambulie na tuliona kwa dakika 20 za kipindi cha kwanza namna wachezaji walivyocheza kwa nguvu. Nimsifu, Farid kwa namna alivyocheza kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi. Kijana huyo alijiamini licha ya kuwa alikuwa akiichezea kwa mara ya kwanza timu ya Taifa. Ni kielelezo cha vipaji vya Kitanzania. Farid alimfanya Mkwasa aonekane bora pia kwa kuamua kumuanzisha yeye badala ya John Bocco, Saimon Msuva, Deus Kaseke.
Udhaifu pekee wa timu ambao Mkwasa anapaswa ku-dili nao ni pasi za mwisho. Viungo wote watatu, Farid, Mudathir na Himid walicheza kwa umakini mkubwa na kuipandisha timu mbele lakini miongoni mwao hakuna aliyeweza kupiga pasi ya mwisho. Kama, Mudathir atajifunza kwa kinda mwenzake, Said Ndemla namna ya kupiga pasi za kupenyeza atakuwa kiungo bora zaidi.
Ndemla aliingia kipindi cha pili badala ya Mudathir na akawa mzigo mpya kwa safu ya kiungo ya Nigeria. Alipiga pasi za mbali na hivyo kuifanya Stars kuwa na kasi zaidi dakika za mwisho. Ni kama sub za kuwaingiza Ndemla, Bocco na Msuva zilichelewa kutokana na kuifanya timu kucheza vizuri zaidi mwishoni lakini katika hali ya kawaida kazi iliyofanywa na Mudathir na Farid ni kipekee na ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa timu. Mkwasa alifanya kila kitu katika muda mwafaka na 'kamari zake zote akilishinda', kuanzia katika upangaji wa timu hadi katika 'sub'.
Mkwasa atakuwa na wigo mpana wa kutazama wachezaji wapya katika ligi ili kutatua tatizo hilo. Mwalimu huyu wa muda sasa angepewa mkataba wa miaka mitatu ili afanye kitu kikubwa katika timu ya taifa ya Tanzania. Ni mwalimu 'spesho' kwetu na tunapaswa kumtumia kwa uhakika na si kama 'spea tairi'.
Chad kapigwa 5-1 nyumbani na Misri iliyo katika kiwango cha juu. Itapendeza Stars ikichukua pointi zote 6 dhidi ya timu hiyo ya Afrika ya Kati. Sare dhidi ya Misri na Nigeria katika gemu za marejeano zitaongeza pointi 9 ambazo zitatosha kwenda Gabon. Tumepangwa kundi gumu lakini tayari tuko katika mapambao. Nigeria ni mabingwa wa Mwaka juzi tu, usisahau hilo.
Comments
Post a Comment