MAMBO MUHIMU AMBAYO LAZIMA UYAJUE KABLA YA MECHI YA SIMBA VS YANGA


MAMBO MUHIMU AMBAYO LAZIMA UYAJUE KABLA YA MECHI YA SIMBA VS YANGA

Simba vs Yanga picLeo ni siku ambayo ilikuwa ikisubiriwa sana na mashabiki wengi wa soka la Tanzania, leo ndio siku ambayo unapigwa mtanange wa Dar es Salaam Darby (Yanga vs Simba) mechi hii inatajwa kuwa miongoni mwa Derby kubwa barani Afrika lakini ikiwa ni Derby yenye upinzani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Simba na Yanga zinakutana leo kwenye raundi ya nne ya VPL lakini ikiwa ni mechi ya kwanza inayozikutanisha timu hizo msimu huu, hapa chini nimekuwekea vitu muhimu unavyotakiwa kuvijua kabla ya mechi haijapigwa ili wakati wa mchezo utapofika unakuwa unajua vizuri nini kinaendelea.

Matokeo ya timu zote msimu huu mpaka sasa

Baada ya mechi tatu kuwa zimechezwa hadi sasa, timu zote zimeshinda michezo yote mitatu Simba imeshinda mechi zake dhidi ya African Sports na Mgambo JKT ugenini kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga mechi yao ya tatu walishinda wakiwa kwenye uwanja wa taifa dhidi ya Kagera Sugar. Yanga mechi zao zote wameshinda wakiwa kwenye uwanja wa taifa dhidi ya Coatal Union, Tanzania Prisons na JKT Ruvu.

Vita ya Hamisi Kiiza vs Amis Tambwe

Hawa ni washambuliaji wawili ambao leo watakuwa wakicheza dhidi ya vilabu vyao vya zamani. Kiiza alikuwa Yanga kwasasa yupo Simba wakati Tambwe alikuwa Simba na sasa yupo Yanga na wote kwa pamoja wamekuwa na moto wa ajabu katika kutupia kambani msimu huu.

Kiiza

Mpaka sasa anaongoza kwa kutupia nyavuni akiwa amefunga bao tano baada ya kufunga kwenye mechi ya kwanza bao moja, mechi ya pili bao moja na mechi ya tatu bao tatu na hii ikiwa ni hat-trick ya kwanza kwa msimu huu lakini ikiwa ni hat-trick yake ya kwanza pia akiwa Msimbazi.

Tambwe

Amefunga jumla ya bao tatu hadi sasa. Alifunga bao moja kwenye mechi ya kwanza, halafu mechi ya tatu akatupia mbili dhidi ya JKT Ruvu wakati Yanga ilipoibuka na ushindi wa goli 4-1.

Mtiririko wa matokeo

Yanga

Walianza kwa ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Coasta Union, wakapata ushindi wa goli 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons na mechi ya tatu wakashinda kwa goli 4-1 dhidi ya JKT Ruvu. Leo wanakutana na 'mnyama' hii ina maana kama wanaendelea kwa mfululizo huo wataibuka na goli tano.

Simba

Walianza kwa ushindi wa goli 1-0 dhidi ya African Sports kwenye mechi ya kwanza, mechi ya pili wakashinda kwa goli 2-0 dhidi ya Mgambo JKT na mechi ya tatu wakaibuka na ushindi wa goli 3-1 dhidi ya Kagera Sugar. Kama wataendelea na mfululizo huohuo inamaana leo watafunga bao nne.

Magoli ya kufungwa

Kila timu imeruhusu goli moja kwenye mchezo wake wa tatu, timu zote zimefungwa kwenye uwanja wa taifa ambao zinautumia kama uwanja wao wa nyumbani na kila timu imefungwa kwenye mchezo iliopata ushindi mkubwa.

Yanga

 Imefungwa goli moja wakati ilioibuka na ushindi wa goli 4-1 dhidi ya JKT Ruvu mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa taifa. Yanga wamefunga magoli tisa kwenye mechi tatu walizocheza.

Simba

Ilifungwa goli moja kwenye ushindi wake mkubwa msimu huu hadi sasa ilipoifunga Kagera Sugar kwa goli 3-1 kwenye uwanja wa taifa wakati wao wakiwa wamefunga jumla ya magoli sita hadi sasa.

Historia ya timu hizo kwenye mchezo wa Dar es Salaam Derby

Timu hizi tayari zimekutana mara 79 kwenye mechi za ligi kuu Tanzania bara, mchezo wa leo utakuwa ni wa 80 huku ukiwa ni wakwanza kwenye msimu huu wa 2015/16.

Takwimu zinazungumaje?

Mabinwa watetezi wa ligi hiyo timu ya Yanga wanaongoza kwa kuwafunga watani zao Simba wakiwa wameshinda mechi 29 kati ya 79 wakati Simba wao wameifunga Yanga kwenye mechi 23 kati ya 79 huku mechi mechi 27 kati ya 79 zikiwa nisare.

Matokeo ya msimu uliopita

Kwenye mechi ya kwanza msimu uliopita timu hizo zilitoka sare lakini mechi ya pili (marudiano) Simba iliitandika Yanga kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa Uganda Emanuel Okwi.

Maswali mawili ya kujiuliza kabla ya mchezo wa leo

1. Je, Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara watalipa kisasi cha kufungwa mara kwa mara siku za hivi karibuni au Simba wataendelea kupeleka kilio Jangwani?

2. Je, ni nani kati ya Kiiza na Tambwe atakaepeleka kilio kwenye timu yake ya zamani?



Comments