Baada ya beki wa kushoto wa            Manchester United, Luke Shaw, kuvunjika mguu wa kulia na            kulazimika kuwa nje ya dimba kwa miezi sita, sasa Marcos Rojo            njia nyeupe kurejea kwenye kikosi cha kwanza.
        Shaw alipigwa daluga kali na            Hector Moreno wa PSV Eindhoven ya Uholanzi katika pambano la            kwanza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye uwanja  Phillips jijini Eindhoven            Jumanne usiku, ambako Mashetani Wekundu walilala kwa mabao            2-1, huku ikimpoteza beki huyo dakika ya 18.
        Kocha wa Man United, Louis van            Gaal, alifichua kuwa Shaw mwenye umri wa miaka 20, alikuwa            akilia hadi vyumba vya matibabu na baadae vyumba vya kuvalia,            pale alipoambiwa kwamba atakuwa nje ya uwanja kwa miezi sita.
        Marcos Rojo beki wa kimataifa wa            Argentina aliyekuwa na mgogoro na Van Gaal aliingia kuchukua            nafasi ya Shaw.
        Van Gaal amesema kuumia kwa Shaw            ni pigo kubwa lakini akajipa moyo kuwa uwepo wa Rojo utasaidia            kufunika pengo.
        Kurejea kwa Rojo kunamaanisha            kuwa Daley Blind atalazimika kwenda kucheza beki ya kushoto            huku Rojo akiungana na Chris Smalling kuunda pacha ya beki ya            kati.
        "Mimi si daktari, ndio maana            nakosa kauli rasmi ya lini atarudi uwanjani, lakini kimsingi            unapovunjika mifupa miwili mikubwa, unakuwa na nafasi kubwa ya            kupona baada ya miezi sita," alisema Van Gaal akionesha            simanzi juu ya Luke Shaw.
        Kabla ya Jumanne, Rojo hakuwa amecheza hata mchezo            mmoja wa Manchester United msimu huu.
                                        
Comments
Post a Comment