KITWANA MANARA ATOA LA MOYONI KUHUSU WACHEZAJI WA KIGENI


KITWANA MANARA ATOA LA MOYONI KUHUSU WACHEZAJI WA KIGENI

MSHAMBULIAJI na kipa mahiri wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Kitwana Manara 'Popat' amesema kuwa umefika wakati kwa Makocha wa Ligi Kuu kuwapa nafasi zaidi wachezaji wazawa kuliko kuwabeba wageni.

Manara aliseyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kuwa amegundua baadhi ya wachezaji wakutoka nje ya nchi uwezo wao mdogo.

"Kweli wapo wachezaji wamesajiliwa kutoka nje ya nchi uwezo wao ni mdogo, lakini wapo wachezaji wazawa wana uwezo mkubwa ila hawapewi nafasi," alisema Manara.

Amewaomba makocha hao kutoa nafasi zaidi kwa wachezaji wazawa, ili waweze kuonyesha viwango kwenye michuano hiyo.

Gwiji huyo amewasihi wachezaji wazawa nao kujituma ili kuwafunika wageni kwani kinyume chake wataishia kucheza timu za madaraja ya chini, kwa kuwa soka la sasa ni biashara hakuna klabu itakayokubali kukaa na wachezaji mizigo.

"Hebu wachezaji wetu hapa nchini wabadilike na wajitume, wasikubali kuozea benchi, wahakikishe wanapigania namba kwenye vikosi vya kwanza," alisema.

Alisema matatizo ya wachezaji kutojituma na kuozea benchi, yanaighalimu nchi kwa timu ya taifa kutokuwa na wachezaji wenye uwezo na wanaojiamini uwanjani, hivyo kufanya vibaya kila kukicha.



Comments