JE, NI KWELI LIGI KUU ENGLAND BORA ZAIDI BARANI ULAYA?


JE, NI KWELI LIGI KUU ENGLAND BORA ZAIDI BARANI ULAYA?

European-Leagues

Na Simon Chimbo

Kumekua na ubishani usio na mwisho wa kuhusu ipi ni ligi bora barani Ulaya. Kila mmoja amekua akiongea kufuatana na anachokiamini, lakini hebu leo tuanzie hapa nilipojaribu kuchambua utofauti wa ligi hizi.

Pamoja na matangazo ya televisheni kutuambia ligi kuu nchini England Ni bora duniani lakini, uhalisia unabaki kuwa ligi hiyo inapitia kipindi kigumu hivi sasa.

Kuhangaika kwa vilabu vya Uingereza katika michuano ya klabu bingwa Ulaya kwa misimu miwili hivi sasa inatuonesha namna gani ligi hiyo inakosa kujiamini na ubora wake kwa namna nyingine umepungua kiasi.

Utawala wa vilabu vya Bundesliga, mwaka juzi na sasa Hispania, huku kukikosekana timu ya kutoka England katika hatua ya robo fainali barani Ulaya inatia shaka ubora wa ligi hii yenye mashabiki lukuki.

Lakini pamoja na  kushuka kwa ubora wa ligi hii, kuna kitu cha pekee zaidi hakipo katika ligi kuu za mataifa mengine barani Ulaya, nacho ni ushindani.

Nchini Hispania, ukiacha England msimu wa 2013-14 pekee ambapo Atletico Madrid walijitutumua na kutwaa ubingwa lakini bado kuna utawala wa vilabu viwili tu vya Barcelona na Real Madrid.

Ujerumani, kadhalika tangu Borrusia Dortmund ianze kuporomoka, imebakia ni ligi ya timu moja tu, Bayern Munich. Huku pia kukiwa hakuna jipya Ufaransa kwa utawala wa PSG.

PSG ametwaa makombe ya ligi kuu nchini humo mara tatu mfululizo, na  hakuna dalili ya ushindani kutoka timu nyingine hivi karibuni.

Nchini England, timu tano tofauti zimetwaa ubingwa kwa kipindi cha miaka 23. Manchester United, Manchester City, Blackburn Rovers, Chelsea na Arsenal zote zimeonja ladha ya ubingwa.

Kikubwa hapa England ni jinsi bingwa anavyopatikana, points nyingi zaidi zinatakiwa kutwaa ubingwa. Lakini pia ushindani wa timu zinazogombana kubakia kwenye ligi pia ni kitu kingine tofauti cha kipekee.

Lakini kutokufanya vizuri  kwa timu za England barani Ulaya ni pamoja na ukweli kwamba timu hizi hazisajili wachezaji wazuri sana ukilinganisha na ligi nyingine.

Chelsea ni mabingwa watetezi wa ligi nchini England lakini wamemuongeza golikipa Begovic, mshambuliaji Radamel Falcao na Pedro wakiwa wachezaji pekee wenye majina makubwa. Ni ngumu kutetea ubingwa ama kuongeza kitu klabu bingwa Ulaya. Wakati Bayern Munich wamemsajili moja ya viungo bora barani Ulaya Arturo Vidal na Douglas Costa.

Barcelona mabingwa wa makombe matatu msimu uliopita wamezidi kujiimarisha kwa kumuongeza Arda Turani. Wakati huo huo PSG wamemsajili Angel Di Maria.

Kila mtu alishuhudia namna Manchester United ilivyopotea barani Ulaya baada ya kumuuza Cristiano Ronaldo na kumpoteza pia Carlos Tevez huku wakiwafidia kwa Antonio Valencia na Michael Owen.

Hapa ndipo timu za England zinakwama kwa kiasi kikubwa, Chelsea walikua vizuri  wakiwa na kikosi kizito cha Michael Ballack, Frank Lampard na Makelele katikati ya uwanja. Leo hii ni ngumu kuwatishia nyau Real Madrid wenye Ronaldo, Bale na Modric.

Manchester City imeshindwa kuendelea kuwa sawa tangu kupoteza nyota wake wengi kama Gareth Barry, Nigel De Jong na sasa wameshindwa kumsajili Paul Pogba, tutegemee nini klabu bingwa Ulaya.

Tukimalizia na Arsenal, nani hajui siri ya kilichowafikisha fainali ya klabu bingwa Ulaya 2006? na kupoteza kwa taabu sana mbele ya Barcelona. Huwezi kumfidia Thierry Henry na Emanuel Adebayor, ama Mertesacker na Sol Campbell ukaendelea kuwa sawa.

Mwisho kabisa, huo ndio utofauti wa ubora wa ligi kuu za barani Ulaya, ingawa mjadala juu ya ipi ni ligi bora zaidi ni endelevu na hauwezi kuisha pasipo vigezo.



Comments