Sir Alex Ferguson anaamini Manchester United itatwaa taji la ligi baada mlinda mlango David de Gea kuongeza mkataba wa muda mrefu kwenye klabu hiyo.
De Gea alikuwa anakaribia kuikacha Manchester United na kutua Real Madrid lakini uhamisho wake uliingia dosari dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya joto.
Muda mfupi baada ya dili kukwama, De Gea alisaini mkataba mpya utakao muweka Old Trafford kwa miaka minne ijayo kitu ambacho Ferguson anaamini kinaongeza nafasi ya Manchester kutwaa ubingwa wa EPL.
"Nadhani De Gea atatushindia taji la ligi", alisema Ferguson
Ferguson alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kuhusu mambo mengine mengi alipokuwa akifanyiwa mahojiano ambayo yalichukua takribani saa moja mbele ya umati wa watu wanaokadiriwa kufikia 2,000 kwenye ukumbi wa Bridgewater Hall jijini Manchester siku ya Ijumaa usiku.
"Tuko nafasi ya pili kwenye ligi", alisema Ferguson ambaye alishinda mataji 13 ndani ya miaka 26 aliyodumu ndani ya Old Trafrord.
"Tupo kwenye nafasi nzuri kwasababu wanaoongoza ligi (Manchester City) hawajapoteza mechi hata moja hadi wiki iliyopita wakati United ilishinda dhidi ya Southampton na mambo yakabadilika.
"Chelsea wamepoteza michezo kadhaa, Arsenal wamepoteza pia, kama unaendelea kuwa kwenye nafasi hiyo hadi mwaka mpya unakuwa na nafasi nzuri".
Ferguson pia anaamini usajili wa Anthony Martial utaisaidia United kunyanyua ndoo ya ligi ya EPL mwezi Mei mwakani.
Comments
Post a Comment