BENZEMA AIPELEKA MADRID KILELENI LA LIGA, RONALDO AKWAMA KUVUNJA REKODI


BENZEMA AIPELEKA MADRID KILELENI LA LIGA, RONALDO AKWAMA KUVUNJA REKODI

Karim BenzemaKarim Benzema amefunga magoli mawili yaliyoipeleka Real Madrid kileleni mwa La Liga baada ya kuibuka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Athletic Bilbao.

Benzema sasa amefikisha jumla ya magoli matano kwenye ligi ya Hispania msimu huu, alifunga goli la kwanza akitumia makosa ya beki Mikel San Jose aliyekuwa akimrudishia mpira golikipa wake.

Golikipa wa Madrid Keylor Navas alikaribia kuvunja rekodi ya 'clean sheet' kwenye klabu hiyo iliyowekwa miaka 40 iliyopita lakini Sabin Merino aliisawazishia timu yake na kuharibu mipango hiyo.

Benzema aliifungia Real Madrid goli la pili na kuipeleka timu yake hadi kileleni mwa msimamo wa La Liga kufuatia kichapo walichokipata Barcelona cha goli 4-1 mbele ya Celta Vigo.

Cristiano Ronaldo amebakiza magoli matatu ili avunje rekodi ya kuwa mfungaji mwenye magoli mengi ndani ya klabu hiyo inayoshikiliwa na Raul Gonzalez lakini leo ametoka kavu.

Nyota huyo wa Ureno aliingia uwanjani akiwa na jumla ya magoli 321 aliyoifungia Madrid kwenye michuano yote lakini alijikuta akitoka nje ya uwanja bila kutikisa nyavu.



Comments