Tamasha la kimataifa la Sauti Za Busara halitafanyika mwakani (2016)



Tamasha la kimataifa la Sauti Za Busara halitafanyika mwakani (2016)
Tamasha la muziki la kimataifa, Sauti Za Busara ambalo limekuwa likifanyika mwezi wa pili Zanzibar, halitakuwepo mwakani 2016 kutokana na uhaba wa fedha.
sauti
Hii itakuwa ni mara ya kwanza ndani ya miaka 13 Zanzibar kulikosa tamasha hilo lifanyikalo kila wiki ya pili ya mwezi Februari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotions, Yusuf Mahmoud amesema;

"Uamuzi huu haukuchukuliwa kwa wepesi. Kawaida huwa tunatangaza tarehe za tamasha mwaka mmoja kabla. Lakini baada ya kufanya tamasha lililopita kwa mafanikio, tumekuwa katika hali ya ukosefu wa fedha kwa toleo lijalo la 2016. 

Tulijiwekea malengo ya kukusanya dola za kimarekani 200,000 kabla ya Julai, wakati tulipokuwa na matumaini ya kutangaza tarehe za Sauti za Busara 2016. Baada ya mikutano mingi na wadau, tulisogeza muda wetu wa kutafuta fedha hadi usiku wa Agosti 19. Kiasi ambacho tuna uhakika wa kukipata kuandaa tamasha lijayo kwa sasa kinasimamia kwenye dola za kimarekani 42,000, hivyo basi bado tuna safari ndefu mbele yetu.
Kawaida wakati kama huu, tunakuwa tumeshafika mbali kwenye makubaliano ya mikataba mbalimbali kama ya kukodi ukumbi, ukodishaji wa vifaa, wasanii na mameneja, tunaanza kupanga ratiba, maandalizi ya usafiri na malazi kwa wasanii mapema iwezekanavyo. Shinikizo zaidi, tumekuwa tukipokea maswali kutoka kwa watu mbalimbali duniani kote wakitaka kujua tarehe za tamasha ili waweze kufanya mipango yao ya safari. Mauzo ya tiketi za Sauti za Busara haijawahi kuwa tatizo, lakini hii inasaidia kulipa 30% ya gharama za tamasha".
Yusuf ameendelea, "Matamasha yanahamasisha vijana kupenda utamaduni wao, hutoa fursa kwa wasanii na wataalamu wa muziki kukutana na kujifunza , yanashawishi uhai wa tamaduni, pia yanatoa nafasi za ajira kwa watu wa ndani na kutoa mifano ya utalii ambayo inathamini na kuheshimu utamaduni wa ndani. Hata hivyo, tangu mwaka 2004 hatuna msaada wowote wa kifedha kutoka serikali ya Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pamoja na jitihada nyingi, msaada kutoka kwa wahisani, balozi na wafanyabiashara unazidi kupungua siku hadi siku. Busara Promotions ni shirika lisilo la kiserikali; tamasha haliko kibiashara. 

Wengine walipendekeza tujaribu kuomba pesa kupitia mitandao. Hata hivyo, kwa kweli ili kuwa endelevu zaidi, kipaumbele chetu kabla ya toleo la 2017 kitakuwa ni kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na wadhamini na wafadhili ambao wanakubaliana na mtazamo wetu. Mtu yeyote anaesoma ujumbe huu na ana nia ya kusaidia kuiweka Sauti za Busara hai, kukuza ajira nchini, wakati tunaendelea kuung'arisha muziki wetu wenye utajiri wa mila na kukuza utalii wa kiutamaduni Zanzibar na Tanzania, tafadhali awasiliana nami kupitia Busara Promotions."
Chanzo: Michuzi Blog


Comments