MAISHA ni malengo na ndicho kinachomtofautisha binadamu mmoja na mwingine. Na ndiyo tofauti ya straika wa Azam, Herman Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast na wachezaji wengine wanaocheza nafasi kama yake.
Ni straika mwenye akili anayejua nini kimempandisha ndege kwa muda wa saa nane kutoka mjini Abidjan, Ivory Coast mpaka jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Alipoanza msimu malengo yake ilikuwa ni kufunga mabao 20 na akamaliza na mabao 17. Anasikitika kwa hilo lakini bado ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013.
Aliwaacha mbali wanaomfuata kama Mrundi Didier Kavumbagu wa Yanga aliyemaliza na mabao 10, Paul Nongwa wa JKT Oljoro ana mabao nane sawa na Amri Kiemba wa Simba, Jerry Tegete wa Yanga na Hussein Javu wa Mtibwa Sugar.
Kavumbagu ndiye alikuwa tishio mzunguko wa kwanza ambao alifunga mabao saba lakini mzunguko wa pili makali yake yakapungua na akafunga mabao matatu tu na kumpa mwanya Tchetche kuzidi kupaa kileleni msimu huo.
Tchetche anakumbukwa na mashabiki wa soka alipokuja kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam na timu yake ya taifa ya Ivory Coast kushiriki mashindano ya Cecafa.
Mchezaji huyo mwenye umbo lenye misuli mikubwa na aliyejazia vilivyo sehemu ya kifua, mikono, mapaja na vijumbulu hali inayomfanya kuwa tishio kwa mabeki wapinzani.
Ana sifa ya kupiga mashuti makali na aina ya mabao yake ni kupitia pembeni kwenye engo, kati na mbali.
Alipofanya mahojiano na tovuti hii, Tchetche anasema: "Namshukuru Mungu kwa kunifanya kuwa mfungaji bora, hii isingewezekana bila mchango wa wachezaji wenzangu, makocha na mashabiki," alisema Tchetche.
Techeteche sasa ana misimu mitatu Azam FC na katika kipindi chote hicho amekuwa mchezaji nyota wa klabu na ligi. Msimu wa 2013/14 Tchetche alishinda tuzo ya mchezaji bora wa kigeni anayecheza kwenye VPL.
Shukrani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na wachezaji wenzangu na benchi zima la ufundi kwa ushirikiano wao,
anasema Tchetche, ambaye ni shabiki wa Manchester United.
Na nafikiri nimeshindwa kufikia malengo yangu kwa sababu ya majeruhi. Nilikuwa sikuwa na wakati mzuri misimu miwili iliyopita kwa sababu ya kuandamwa na majeruhi nikawa sichezi mechi mara kwa mara. Lakini sasa nipo vizuri na natarajia kurejesha makali yangu msimu ujao anasema.
Kocha wake, Hall aliwahi kusema: "Tchetche ni mchezaji mzuri ana kipaji na nguvu za mpira kiujumla ni msaada katika timu. Anacheza kitimu na kwa ushirikiano dhidi ya wenzake na anafuata maelekezo unayompa,' anafafanua Hall.
Matatizo ya Tchetche ni kama ya washambuliaji wengine. Kuna sehemu ambazo ni rahisi kufunga huwa anakosa na nyingine ni ngumu kufunga yeye anafunga na kwangu nachukulia ni kawaida tu,
anasema Hall.
Nje ya soka
Tchetche ambaye alifika nchini akiwa anazungumza lugha moja tu ya Kifaransa, lakini sasa anaongea kwa kujitahidi Kiingereza na Kiswahili.
Anasema, anafurahia maisha ya Tanzania kwa sababu ameshakuwa mzoefu na mazingira:" Awali ilikuwa ngumu kwa sababu ya ugeni lakini sasa nimezoea."
Tchetche amekuwa mpenzi wa chapati na mchuzi, ugali na kuku na anasema anakifurahia aina hiyo ya msosi.
Awali akiwa Ivory Coast alizoea chakula chao cha asili cha Aloco. Aloco ni ndizi zinazokaushwa wao wanakula na samaki.
Historia
Katika familia ya Tchetche wamezaliwa sita. Watatu kati yao ni wanaume na watatu ni wanawake.
Yeye ni uzao wa pili ambao wamezaliwa wawili pamoja na pacha wake, Michael Kipre Bolou. Kaka yao ni Oscar Kipre Patrick na ndugu zake wakike ni Kipre Larine, Kipre Josiane na Kipre Andrea.
Anatoka katika kabila la Bete na amezaliwa na kukua katika kijiji cha Issia, Daloa, Ivory Coast. Kipre ameoa na ana motto anayeitwa, Kipre Astride.
Chanzo Mtandao wa Azam fc.
Comments
Post a Comment