MFAHAMU PASCAL SERGE WAWA ALIYEPAMBANA NA KINA MESSI, ODEMWINGIE, DI MARIA NA KUN AGUERO


MFAHAMU PASCAL SERGE WAWA ALIYEPAMBANA NA KINA MESSI, ODEMWINGIE, DI MARIA NA KUN AGUERO

Serge Pascal Wawa ni jina lililojizolea umaarufu mkubwa kwenye michuano ya Kagame Cup 2015 iliyomalizika jana kwa Azam kuchukua ubingwa wa kombe hilo ilipokutana na Gor Mahia ya Kenya na kuicharaza kwa kwa bao 2-0 kwenye mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Azam kutangazwa mabingwa wapya wa kombe hilo.

Pascal Wawa ni nani?
WAWA
Wawa ni beki wa kati wa Azam FC inayoshiriki ligi kuu ya Tanzania bara, (Vodacom Premier League) amezaliwa Januari 1, 1986 Bingerville, Ivory Coast. Wawa alianza kucheza mpira mwaka 2003 kwenye Academy ya ASEC Mimosas ambyo imezalisha wachezaji wengi wa kiafrika wenye majina makubwa barani Ulaya na duniani kwa ujumla. Bonaventure Kalou, Didier Zokora, Emmanuel Eboué, Gervinho, Salomon Kalou, Romaric,Didier Ya Konan na Yaya Touré ni baadhi ya majina ya wachezaji walitoka ASEC Mimosas.
January 19, 2009 Wawa alienda kufanya majaribio kwenye klabu ya FC Lorient ya nchini Ufaransa lakini mwaka 2010 alijiunga na miamba ya soka ya Sudan timu Al-Merrikh kwa mkataba wa miaka mitatu. Na Novemba 2014 Wawa alijiunga na timu ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam.
Je, Wawa meshawahi kuitumikia timu ya taifa ya Ivory Coast?
Wawa alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa ya Ivory Coast waliocheza michuano ya Olympic iliyofanyika mwaka 2008 mwaka huo michuano hiyo ilipigwa Beijing, China kuanzia Agosti 7 mpaka Agosti 23, Wawa alipata nafasi ya kucheza jumla ya mechi nne ambazo Ivory Coast ilicheza kwenye mashindano hayo.
Ivory Coast ilipangwa Kundi A pamoja na timu za Argentina, Australia, na Serbia. Kwenye kundi hilo Ivory Coast ilimaliza ikiwa ya pili nyuma ya Argentina walioongoza kundi wakiwa na pointi tisa wakati Ivory Coast ikimaliza ikiwa na pointi sita baada ya kushinda michezo miwili ilipokutana na Serbia ambapo ilishinda kwa goli 4-2 na ushindi mwingine ukiwa dhidi ya Australia wa goli 1-0 wakati ilipoteza mchezo wake dhidi ya Argentina kwa goli 2-1.
Mchezo wa kwanza wa Ivory Cost ulikuwa dhidi ya Argentina, Wawa alikuwa ni sehemu ya kikosi kilichoanza dhidi ya timu ngumu iliyojaa nyota wa kila aina wenye majina makubwa duniani. Kikosi cha Argerntina kiliundwa na washambuliaji kama Lionel Messi, Sergio Aguero, Di Maria na Lautaron Acosta lakini Wawa akamudu kucheza na kuwakaba huku timu yake ikipoteza mchezo huo kwa goli 2-1.

Mechi ya pili Wawa alikuwepo kwenye kikosi cha kwanza kilichoinyuka Serbia kwa goli 4-2 akikabiliana na wakali kama Miljan Mrdakovic, Aleksandar Zivkovic, Nenad Tomovic na Zoran Tosic wakati huo akimuweka benchi Souleymane Bamba ambaye alitamba kwenye michuano ya kombe la dunia 2014 na mataifa ya Afrika 2015 kwenye kikosi cha kwanza cha Ivory Coast.
Ivory cost ilicheza mechi yake ya mwisho kwenye hatua ya makundi dhidi ya Australia na kuibuka na ushindin wa goli 1-0 na kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya mihuano ya Olympic, kama kawaida Wawa alianza kwenye kikosi cha kwanza akikutana na washambuliaji wa Astralia kama Nikita Rukavytsya, Billy Celeski, Matt Simon akafanya vizuri na kuipeleka timu yake hatua ya robo fainali.
Mechi ya robo fainali Ivory Coast ilikutana na Nigeria ambapo Ivory Coast ikafungwa kwa goli 2-0 na kuondoshwa kwenye mashindano hayo. Serge Wawa alikuwa sehemu ya kikosi cha Ivory Coast kilichoanza lakini akapumzishwa dakika ya 87 kumpisha Abraham Guie-Guie. Kikosi kilichoitoa Ivory Coast kilikuwa na washambuliaji kama Peter Odemwingie na Efe Ambrose na wote hao walikabwa na Wawa.

Kwanini Wawa ameonekana beki bora kwenye michuano ya Kagame 2015?
Wawa ana uzoefu wa michuano ya kimataifa, kushiriki kwake kwenye michuano ya Olympic 2008 na kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza kulimpa uzoefu wa hali ya juu. Kwenye michuano ya Olympic alikutana na washambuliaji bora Ulaya na duniani, amlikutana na washambuliaji kama Messi, Aguero, Di Maria, Odemingie na wengine wengi ambao alimudu kuwakaba na kuzidi kujifunza mbinu mpya za kukabiliana na wachezaji wenye viwango vya juu. Lakini amecheza michuano ya Afrika ngazi ya vilabu akiwa na klabu yake ya zamani (Al Merrikh) na kupambana na washambuliaji hatari barani Afrika.

Kujituma
Muda wote awapo uwanjani Wawa ameonekana kuwa ni mchezaji anaejituma wakati wote wa mchezo, anatumia nguvu pale inapohitajika lakini vilevile anatumia akili nyingi pale anapolazimika kufanya hivyo hasa anapokuwa anamkaba mchezaji ndani ya eneo lake la hatari. Anapokutana na mshambuliaji asiyeweza kupambana inakuwa ni kazi rahisi kwake kuondoka na mpira kirahisi.
Nidhamu
Wawa amekuwa tofauti na mabaki wengi wa Tanzania, Afrika Mashariki na Kati na hii inatokana na uzoefu na kujitambua kuwa yeye ni mchezaji wa kimataifa. Ni marachache sana amefanya faulo pale anapomkabili mpinzani wake na hiyo imepelekea kuzuia kadi ambazo si za lazima kwake. Hajawahi kuhusishwa vibaya kwenye maisha yake ya nje ya uwanja tofauti na wachezaji wengine wanaopata pesa nyingi kutokana na mishahara yao.
Aina ya wachezaji aliokutana nao kwenye kombe la Kagame.

WAWAAAA
Kwenye kombe la kagame amekutana na wachezaji ambao kwake ni wakawaida sana na akaweza kuwamudu vyema kiasi cha kuwafunika na kujiolea tuzo za man of the match kila kukicha. Timu yake ilipokutana na Gor Mahia wadau wa soka wakawa wanasubiri kushuhudia vita kati ya Wawa dhidi ya Olunga mshambuliaji wa Gor Mahia aliyeibuka mfungaji bora wa michuano hiyo. Lakini mambo yalikuwa tofauti kwasababu Olunga alishindwa kutamba mbele ya Wawa. Wawa amekaba akina Aguero wanao wasumbua akina John Terry Ulaya, Messi na wengine wengi.
Anakutana na Malimi Busungu wa Yanga ambaye hajacheza bado soka la kimataifa kwa Wawa inakuwa ni kazi ndogo sana kumdhibiti. Hali kadhalika kwa Mateo Anthony wa KMKM na Kondo Shabani mshambuliaji wa KCC FC ya Uganda ambae mpaka mashindano ya Kagame yamemalizika hakufunga goli hata moja. Hao wote walishindwa kufurukuta pale walipokutana na mziki wa Serge Pascal Wawa.
Huyo ndie Paccal Wawa mchezaji aliyetwaa tuzo ya beki bora wa mashindano ya Kagame na kuchukua tuzo ya man of the match mara tatu ndani ya mashindano ya Kagame Cup na kuiongoza safu ya ulinzi ya Azam kumaliza michuano hiyo ikiwa haijafungwa goli hata moja tangu hatua ya makundi hadi fainali.



Comments