"Daa..! Kaka mambo vipi? Hivi AFC bado haijapandaga ligi kuu tuu? Lowasa na Magufuli vipi… Vipi Tegete naye anapata nafasi ya kucheza Yanga? Kama hapati mwambie aje huku Birmingham hata kwa mkopo, mbona yule dogo wa Barcelona anayecheza kama Pedro kaja huku Villa park kuungana na akina Ayew" Hii ilikuwa meseji ambayo alinitumia rafiki yangu anayesoma pale mitaa ya Witton katika jiji la Birmingham inayopatikana timu ya Aston Villa ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja.
Ujumbe wa huyu jamaa ulinifanya kupata wazo la kumjadili mchezaji aliyezungumzwa kwenye meseji hiyo, japokuwa una shughuli nyingi ni vyema ukitumia muda wako mchache kutazama saini ya mchezaji huyu na mwelekeo wake ndani ya Villa Park, karibu sana.
Tarehe 23 November mwaka juzi, mashabiki wa soka duniani hasa wale wapenzi wa Uefa Champion League walikuwa na mshangao mkubwa baada ya kumuona Gerardo Martino akimtoa Cesc Fabregas na kumuingiza kijana mdogo wa miaka 17 aliyekuwa na jezi namba 27 mgongoni kwenye mechi dhidi ya Ajax. Matumaini ya mashabiki wa Barcelona yalikuwa ni kuhakikisha wanasawazisha magoli mawili na kuongeza goli la tatu, japokuwa siku tatu zilizopita watu walimuona kwenye mechi ya Granada hii haikutosha kumuamini na waliishia kumlaumu 'Tata'. Mechi moja aliyocheza kwenye Uefa Champion League ilimfanya aonekane sehemu mbalimbali za dunia ikiwemo jiji la Birmingham.
Nikiwa sina hili wala lile nilishangaa sana kumuona Kocha kijana, Tim Sherwood akizungumza na shirika la habari la Uingereza, "Ni mtu anaebadilika uwanjani, anacheza kwa kasi na huwezi jua anakwenda kufanya nini muda mfupi baada ya kupata mpira, namaanisha hiyo ni sifa nzuri. Ni rasilimali kubwa kwenye timu yake, ana uwezo wa kushambulia wapinzani na ninafurahi kumsajili hapa" alizungumza kocha huyu mapema kabisa 14/08/2015. Ghafla kumbukumbu zangu zikanirudisha nyuma kwenye mechi ya kombe la mfalme mnamo mwezi December 2014 ambapo Barcelona ilishinda magoli 8-1 dhidi ya timu ya chini kabisa inayoitwa SD Huesca, mechi ambayo kinda huyu alicheza kwa dakika 16 na kufunga goli moja.
Hapa namzungumzia kijana mweusi anayependa sana kusali kama wanavyofanya akina Masoud Ozili, Kourt Zouma na Franky Ribbery. Kinda mdogo mwenye mwili wa wastani ambao kwa huku Tanzania mwili wake unge 'fiti' kwenye kazi zozote za kutumia nguvu ikiwemo kubeba 'zege' na hata kupakua mizigo Kariakoo. Kijana mdogo aliyezaliwa ule mwaka ambao Mama yake Flavian Matata na Watanzania wengine walipoteza maisha kwenye ajali ya Mv Bukoba. Bila shaka Tayari umeshamfahamu Adama Traore Diarra ndiye mtu anaezungumzwa hapa.
Mitaa mbalimbali ya Jiji la Birmangham inazungumza ujio wa Adama ndani ya Villa park hasa katika kipindi hichi ambacho akina Jordan Ayew Scott Sinclair na Micah Richard wametua Villa Park. Binafsi ninaamini Adama ni Mchezaji mkubwa mwenye umri mdogo aliyekulia na kucheza kwenye timu kubwa na sasa anakuja kuendeleza kipaji chake kwenye timu ndogo inayocheza ligi kubwa duniani. Kama umeelewa kauli yangu utakubaliana na mimi kuwa La Masia ni Academy kubwa na yenye kutoa ujuzi mkubwa pengine kuliko Academy yoyote Ulaya.
Adama ameanza kucheza La Masia akiwa na miaka 8 hadi leo anasafiri takribani kilometa 1270 kutoka Barcelona hadi Jijini Birmingham akiwa na miaka 19. Kwa hesabu ya haraka haraka ni kwamba huyu dogo amekaa Zaidi ya miaka 10 pale Camp Nou huku akilala na kuamka ndani ya La Masia. Akili zake uwanjani na mbio zake zilimfanya ajue kupiga chenga kama Pedro, achilia nguvu zake miguuni kama Busquest ila umbo lake pia lilimfanya apandishwe haraka kwenye kikosi cha wakubwa akiwa na miaka 17 pekee. Hapa ndo dunia ya soka ilimtambua kwa haraka zaidi hasa pale kwenye timu ya Taifa ya Uhispania kwa vijana wa umri chini ya miaka 19 ambapo alicheza kama winga msumbufu mno.
Safari yake kwenye ligi ngumu yenye ushindani ndiyo itakayowafanya Barcelona kumuamini na kumrudisha tena Camp Nou kwani hili ni zao lao ambalo bado hawajanufaika nalo kabisa kwani hata pauni milioni 12 walizomuuza kwa sasa ni pesa ndogo mno kwa Barcelona. Wanachokitaka wao ni kumuona Adama siku moja anarudi Camp Nou kwenda kutetea maslahi ya Cataluna. Hili linawezekana hasa kutokana na kifungu kwenye mkataba wao na Aston Villa unaomruhusu Adama kununuliwa tena na Barcelona kama huduma yake itahitajika tena Camp Nou.
Kutokana na kasi, nguvu na uwezo aliokuwa nao Adama naamini mawinga walioanza kwa kasi kama akina Montero na Sterling wajipange upya kwani dogo anajua kulazimisha kupita kwa nguvu alafu anayo ngozi ya ngumu kama ya wale ndugu zake wengine wa kule Mali, Pia nafasi anayokwenda kupewa na Tim Sherwood itawanyamazisha midomo wengi ambao wanamchukulia kawaida mtu aliyelelewa na kukulia jumba la vipaji la pale La masia. Japokuwa alicheza mechi 4 pekee tangu apandishwe kwenye timu ya wakubwa ila kule Segunda Division wanamjua huyu jamaa ni nani.
Hatimaye nahitimisha kwa kutoa hisia na mtazamo wangu kuwa huyu dogo anakwenda Villa Park kuhakikisha Aston Villa wanakuwa salama kwenye ligi na hofu ya kuteremka daraja inaondoka, pia Adama anakwenda kuonesha makali ili Barcelona wamrudishe tena Camp na kama tutakuwa hai naamini tutamshuhudia kwenye vikosi vya wiki mara kibao ndani ya msimu huuna jicho langu la tatu linamuona akiingia kwenye list ya wachezaji wanaowania tuzo ya Mchezaji bora chipukizi huku akiwa sambamba na akina Depay. Kwa lugha ya Kiarabu wanasema 'in shaa allah' ila 'Kibongo bongo' tunasema Mungu akipenda tutaona makubwa sana kutoka kwa Adama, kijana ambaye anamiliki uraia wa Mali na Hispania
Comments
Post a Comment