KWANINI STONES ANAMNYIMA MOURINHO USINGIZI?


KWANINI STONES ANAMNYIMA MOURINHO USINGIZI?

"nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kuhakikisha Tanzania inaanda
michuano yoyote iliyo chini ya CAF kabla sijaondoka ikulu" ningekuwa
na furaha kama ningesikia hata mgombea mmoja tu wa urais ametamka
maneno haya jukwaani..! Ila kwakuwa michezo inachukuliwa kama kitu cha
ziada, hata wanasoka wanachukuliwa pia kama wapiga kura wa ziada…!
Ila nyie mtakaoingia Magogoni msituchukulie "Simple" tambueni michezo
ni muhimu kama sekta za uchumi, usalama na zingine kibao ambazo kila
siku ndio salamu zenu. Anyway tuachane na hayo kwanza hapa sio mahala
pake, naomba tujadili mambo ya msingi katika michezo….

stone

Unapopewa mtihani wa kuwataja Makocha bora 10 kwa sasa duniani, ni
lazima utafeli mtihani huo kama jina la Mreno mkorofi anaependa shari
na ubabe nje na ndani ya uwanja Jose Mourinho halitakuwepo kwenye
list. Mbali na ubora wake kuonekana katika mafanikio aliyoyapata, pia
Wachezaji na Makocha wenzake mara kibao wamekiri Jose ni bora. Naamini
tukijaaliwa ipo siku tutaonesha kauli mbalimbali za Makocha na
Wachezaji juu ya Mreno huyu mwenye majivuno. Kutokana na ubora wake,
Jose pia amekuwa bora kutafuta wachezaji na kutengeneza kikosi bora,
wachezaji wengi waliosajiliwa na Jose huwa bora sana chini yake.

Mifano ipo mingi ila kama wewe ni mfuatiliaji wa soka utagundua kuna
Kinda mmoja anasumbua ubongo wa Jose. Inawezekana Jose huwa halali,
kama analala basi anachelewa kupata usingizi na kama akipata usingizi
basi anamuota Kinda huyu anafanya "Tackle". Ni wazi kuwa mnamjua ni
nani anaezungumziwa hapa, sio mwingine bali ni kijana wa kizungu,
mrefu kiasi ila amejaliwa misuli ya miguu, anajiamini sana na hupenda
kupiga chenga sehemu ambayo hukutarajia.. Hapendi kufuga nywele ndefu
ila mipira mirefu hupenda kuicheza, ni mpiga penati mzuri na ana uwezo
wa kucheza kati na pembeni, hapa namzungumzia John stones…

stone 3

Kijana ambaye jina lake pekee linamuonesha anatoka wapi..! Bila shaka
kwa wale ambao wanasoma historia unapozungumzia majina kama Stones,
Cahill, ni majina halisi ya wale Waingereza "original". Chelsea
imekuwa ikimfukuzia mlinzi huyu kwa kasi na hadi sasa wamekataliwa
mara 2 ila tayari wameongeza dau la 3 ambayo ni kubwa sana kutokana na
umri na nafasi anayocheza Stones. Kwa pamoja leo naomba tuwe wote
tutazame kwanini Chelsea ina mng'ang'ania bwana mdogo huyu wakati bado
ina akiba ya wachezaji wanaocheza nafasi kama yake..? Karibu sana
ndugu msomaji hadi mwisho wa makala hii fupi.

Sababu ya kwanza ni kwamba Stones anaonekana kuja kuwa beki bora
kuwahi kutokea pale England. Watu wa Pwani ambao ndo tunaamini ni
Waswahili "original" wanasema 'nyota njema huonekana asubuhi'. Naamini
kwa wale wapenzi wa Epl walimuona huyu dogo msimu uliopita tangu akiwa
na miaka 20, kiwango chake kilikuwa hatari sana kwani katika mechi 23
alizoanza pale Godson Park msimu uliopita kiwango chake hakielezeki
kwani ndani ya mwaka mmoja amejenga "Partnership" nzuri na mkongwe
Phil Jagielka pale nyuma na kuanza kutajwa kama "World Class
Defender". Amekuwa mzuri sana pale ambapo Everton inashambuliwa…
Kutokana na hili ni wazi Jose anataka aanze kumtengeneza Terry mpya
mapema kabisa kabla hakujapambazuka…!

Jambo lingine linalowasumbua Chelsea ni mashaka na majaaliwa ya
kiwango cha Gary Cahill pale Darajani. Naamini ukiweka unazi pembeni
utakubaliana na mimi kuwa kipigo kitakatifu walichokipata Chelsea siku
ya mwaka mpya cha 5-3 dhidi ya Spurs kilichagizwa na makosa binafsi ya
Cahill, pia mara kibao wameshindwa kuelewana na Cuortois pale nyuma na
wapinzani wamekuwa wakifunga kirahisi. Kwa miaka 3 aliyokaa Chelsea
kacheza kwa mafanikio makubwa akiwa na Terry ila kumekua na makosa
madogo madogo, haya makosa machache ndio yalimfanya asipangwe kwenye
baadhi ya mechi na Zouma kucheza na Terry pale nyuma.

Kama utakumbuka mwezi January Cahill alianza kupata mashaka kutokana
na kiwango cha Zouma, kutokana na haya Chelsea inategemea Stones
atakuwa mbadala mwingine eneo hili, kumbuka Stones ana miaka 21 huku
Cahill akiwa na miaka 29. Ni wazi kuwa kinda huyu akija ata
'wachachafya' wote wanaocheza eneo hili kwani makosa madogo madogo
yamezidi pale nyuma.

stone 2

Sababu nyingine kubwa kabisa ni kutaka kurithi nafasi ya Terry pale
Darajani. "JT" amekuwepo Darajani tangu akiwa na miaka 14, amekuwa
beki aliyefunga magoli mengi pale Epl, msimu uliopita alicheza dakika
zote kwenye mechi zote za Epl, kutokana na miaka 34 aliyonayo ni wazi
msimu ujao unaweza kuwa wa mwisho kwake kucheza kila mechi. Zouma
tayari ameshaanza kumpa changamoto Cahill.! Swali la kujiuliza je ni
nani anaempa changamoto Terry? bila shaka Stones ndiye mchezaji pekee
atakaye kuja kucheza kwa mafanikio kwenye nafasi ya Terry kutokana na
umri na taifa analotoka.

Sababu nyingine ni kwamba anategemewa kuunda "Long partnership" na
Mfaransa Kurt Zouma pale Darajani. Kutokana na Cahill kuanza kupewa
"Challenge" na Zouma mapema ni wazi miaka miwili ijayo Zouma atapata
nafasi ya kudumu..! Hapa ndo atacheza sambamba na Stones. kumbuka
Cahill ana miaka 29 na Terry ana 34, ila Zouma na Stones wote wana
miaka 21, teh teh teh teh..! Umegundua nini hapo?? Kuna watu muda sio
mrefu wanakwenda kuwa watazamaji na kupisha damu changa pale Darajani.
Mou amekuwa akipenda na kusifia kiwango cha Zouma mara kwa mara,
kutokana na hili Stones atafiti sana akiwa na Zouma pale nyuma.

Kitu kingine ni kwamba Stones ni "Resources" ya muda mrefu, Mou
alikuwa ana mwinda Varane kwa muda mrefu sana bila mafanikio, mara
baada ya dili hili kufeli ameangukia kwa huyu mzungu anaezungumza
lugha ya Kiingereza kwa ufasaha.! Ni wazi atakuwepo Darajani kwa miaka
14 ijayo kama atasajiliwa, kwa watu waliosoma mipango kama mimi hapa
timu itapunguza "cost" ya kununua mabeki zaidi kwa Stones pia ana
uwezo wa kucheza pembeni na hata "Defensive midfielder" kama
akipangwa. Pia ni mchezaji wa Ki-ingereza kwa hiyo endapo sheria
zitazidi kubana wachezaji wa kigeni bila shaka hapa Chelsea watakuwa
salama zaidi.

stone 3

Kutokana na kiwango chake kuwa juu mapema sana Kocha wa England
"Under-21″ aliwahi kusema "Ni aina ya wachezaji tunao wahitaji, ni
kama ametokea Ureno na Ujerumani, kila siku tunasema, kwanini
hatuzalishi wachezaji kama hawa" alimaliza Gareth Southgate. Kwa dau
lolote ni wazi Chelsea watampata beki huyu ambaye kwa sasa anavaa jezi
namba 5 kutoka ile 26 ambayo tulikuwa tumeizoea.

Kama mambo yatawaendea vizuri vijana wa "West London" ni wazi kuwa ipo
siku mtakubaliana na mimi kuwa Mourinho ni Kocha mzuri na habahatishi
katika usajili kwani ataandelea kuijenga Chelsea, kumbuka tangu
aondoke Cole, Ze blues inazimisi zile "Tackle" pale mashambulizi
yanapokuwa mengi, pia kumbuka hata timu iliyochukua ubingwa wa Ulaya
karibu robo tatu ya Wachezaji walitengenezwa kipindi cha utawala wa
Mou.! Endapo pia usajili huu utafanikiwa unawezekana ukawa usajili
bora katika klabu ya Chelsea msimu huu. Kila lakher kwa lugha ya
Kiarabu wanasema "in shaa allah" na Kimombo wanasema "if god will"
huku Kiswahili tukisema Mungu akipenda tutaona mwisho wa mbio za
Chelsea juu ya saini ya kinda huyu ambaye amekuwa zaidi ya lulu kwenye
kila kona ya pale magharibi mwa London.

imeandaliwa: Salym Juma

imewezeshwa: www.shaffihdauda.co.tz "The home of exclusive sports news"



Comments