AZAM WANASTAHILI PONGEZI KWA KUENDELEA KUFUTA MAKOSA YA MUDA MREFU WANAYOFANYA SIMBA, YANGA…..


AZAM WANASTAHILI PONGEZI KWA KUENDELEA KUFUTA MAKOSA YA MUDA MREFU WANAYOFANYA SIMBA, YANGA…..

Na Shaffih Dauda
Namshukuru Mungu aliyenivusha salama mwezi Julai na sasa nimeanza safari ya kuipunguza Agosti! jambo la kuvutia ndiyo mwezi ambao ligi ya England, Hispania na nyingine huanza!
Juma hili nimekuwa nikifuatilia Kombe la Kagame linaloendelea jijini Dar es salaam, sitazungumzia matokeo ya timu zote kwasababu makala hii inawatazama zaidi Azam FC.
Nimebahatika kuzitazama mechi zote za Azam za kundi C ikishinda 1-0 dhidi ya KCCA ya Uganda, 3-0 na Malakia FC ya Sudan Kusini na mechi ya mwisho ikiichapa 5-0 Adama City ya Ethiopia.
Pia niliwatazama katika mechi ya Robo fainali ambayo walishinda kwa penalti 5-3 dhidi ya Yanga baada ya suluhu ndani ya dakika 90.
Azam-Kagame-7
Lengo la kuwafuatilia Azam kwa ukaribu ingawa sitazungumzia matokeo yao ya nusu fainali iliyopigwa jana dhidi ya KCCA, ni kuona kama mabadiliko makubwa ya mfumo wa uendeshaji wa timu yameanza kuleta matunda.
Mara nyingi nimekuwa nikiwapigia kelele Azam hasa wanapoleta mambo ya 'kiswahili' , huku wadau wengi wa soka wakiamini ndiyo klabu pekee inayoweza kulibadili soka la Tanzania.
Mapema mwezi Juni mwaka huu, Azam walitangaza mfumo mpya wa utawala wa klabu na kuunda vitengo vyenye watu wenye taaluma husika, ambao tunaamini hawaingiliwi.
kwa faida yako msomaji, Muundo wa uongozi wa Azam FC uko hivi:
Bodi ya wakurugenzi: Hiki ni kikao cha juu kabisa cha maamuzi ya klabu, wajumbe wake wamebaki kuwa wanafamilia wa familia ya Bakhresa. Viongozi na baadhi ya watendaji hualikwa kwenye vikao ili kutoa ripoti za utendaji na sera.
Uongozi: Mwenyekiti wa klabu amebaki kuwa mzee Said Mohammed, huku aliyekuwa katibu mkuu wa muda mrefu tangia klabu ianzishwe, Nassor Idrissa "Father" akiwa Makamu Mwenyekiti. Nafasi ya katibu mkuu ilifutwa. Nafasi ya Ukurugenzi wa Sheria na haki za wachezaji imeendelea kushikiliwa na mwanasheria Shani Christoms.
Watendaji: Mtanzania Saad Kawemba anaendelea kuwa Mtendaji Mkuu wa klabu, huku klabu ikimuajiri Muingereza mwenye asili ya Uganda, Eli Eribankya kuwa Meneja utawala na fedha. Eribankya anasaidiwa na mchezaji wa zamani wa Azam FC Mtanzania, Lackson Kakolaki.

Wachezaji wa Azam FC wakiwa wamembeba kocha wao juujuu              wakishangilia ushindi wa Kagame

Wachezaji wa Azam FC wakiwa wamembeba kocha wao juujuu wakishangilia ushindi wa Kagame

Benchi la ufundi: Stewart John Hall kutoka Uingereza amerejea kwa mara ya tatu kuongoza benchi la ufundi la Azam FC. Hall anasaidiwa na Mganda George Best Nsimbe, huku Mark Philips kutoka Uingereza akiwa kocha wa magolikipa. kocha wa magolikipa aliyedumu kwa muda mrefu Iddi Abubakar anaendelea kuwepo kama msaidizi wa Philips.
Mtaalam wa tiba ya viungo na lishe "Team Physiotherapist and Nutritionist" ni George Adrian Dobre kutoka Romania na Yusuf Nzawila ameendelea kuwa Kit Manager.
Benchi la ufundi la academy: Mario Marian Anton Marinica kutoka Romania anaongoza benchi la ufundi la timu ya vijana akisaidiwa na Mtanzania , Dennis Kitambi na Idd Nassor Cheche. Twalib Mhidin anaendelea kuwa msaidizi wa Team Dr kwa vijana na mtunza vifaa msaidizi vya vijana ni Saleh Sale.

Ukiangalia mfumo huu wa uongozi, Azam wanastahili pongezi kwasababu Stewart Hall na benchi lake la ufundi wanafanya wanavyotaka na hata ukiwatazama wachezaji wanavyocheza kwasasa unaona kabisa hawachezi kwa ajili ya mtu fulani, wanacheza kwa ajili ya benchi la ufundi.

Stewart sio kocha tu bali ni Meneja wa timu, hakika anatupa maana halisi ya Wazungu ya Meneja wa timu.
Meneja anawajibika kuwaongoza wachezaji kama kundi, pia anawajibika 'kum-meneji' mchezaji mmoja mmoja, anatakiwa kujua anahitaji nini, ana mapungufu gani na amsaidiaje ili kupata kilicho bora kutoka kwake.
Mfano mzuri ni wakati Arsene Wenger anajiunga na Arsenal mwaka 1996. Alikuta wachezaji wengi ni wazee wakiwemo Tony Adams, David Seaman, Martin Keown, Mathew Upson, Ray Parlour, Ian Wright na wengineo.
Ili kupata kilicho bora kutoka kwao, Wenger kwa kushirikiana na mtaalam wake vya vyakula ambaye Azam pia wanaye, aliwatengenezea wachezaji 'Menu' ya kula ili waendelee kuwa na nguvu uwanjani.
Wenger alikaa na wake wa wachezaji na kuwapa semina na ratiba ya chakula kwa mcheza mpira, huwezi amini wale, 'wazee wa Arsenal' walichukua ubingwa wa England msimu wa 1997/1998.
Baada ya pale, Wenger akatengeneza falsafa yake, bodi ya Ukurugenzi ikamwambia inataka nini na yeye akajua nini cha kufanya ili Malengo yaweze kutimia nje na ndani ya uwanjani.
Azam imekuwa mfano wa kweli katika hili, bila kugusia matokeo ya Kagame, timu inaonekana kuwa na viongozi sahihi, wasioingiliana kimajukumu na ndio maana wachezaji wanaonekana kuwa huru na kucheza kwa maelekezo ya benchi la ufundi.
Nawaasa Azam waendelea kubaki katika msingi huo na wamwamini Stewart ambaye naamini hajawahi kuwa kocha mbaya zaidi ya wapambe kumharibia kwa wenye timu.
Tukutane Jumamosi ijayo panapo majaaliwa!

Makala hii imetoka jumamosi hii kwenye gazeti la Championi.



Comments