Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Azam FC wako mbioni kufikia makubaliano ya kumrejesha Uganda winga hatari Brian Majwega kwenye kikosi cha mabingwa wa Uganda, KCC FC.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa KCC FC, David Tamale, amesema kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri na kilichobaki ni kuliweka suala hilo katika maandishi tu.
"Ni kweli," amesema katika mahojiano na moja ya mitandao ya michezo ya Uganda. "Tuko katika mazungumzo ya mwisho na yanatia matumaini, kufikia wiki ijayo tutakuwa tumeshalimaza suala hili," ameongeza Tamale.
Amesema mkopo huo unatarajiwa kuwa wa mwaka mmoja, lakini itategemea na uamuzi wa Azam FC.
"Tunawasubiri Azam FC waamue, itakuwa mwaka mmoja au chini ya hapo," amesema.
Majwega alijiunga na mabingwa hao wa Tanzania Bara 2013/14 Desemba mwaka jana, lakini kocha aliyerejeshwa kwa mara ya pili Azam FC, Muingereza Stewart Hall, amekuwa akimweka benchi licha ya kufanya vizuri msimu uliopita akiiwezesha timu kumaliza nafasi ya pili.
Hall amekuwa na imani kubwa na winga kinda Farid Mussa kwenye nafasi ya wingi ya kushoto katika mfumo aliorejea nao wa 3-5-2.
Mganda huyo hakuwa sehemu ya kikosi cha Azam kilichotwaa ubingwa wake wa kwanza wa Kombe la Kagame mwaka huu kutokana na maradhi ya koo.
Comments
Post a Comment