Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
TANZANIA imeporomoka tena kwenye viwango vya ubora wa soka vinavyotolewav na FIFA kila mwezi baada ya leo shirikisho hilo la soka la kimataifa kutoa viwango vinavyoonyesha Tanzania imeshuka kwa nafasi 12 hadi nafasi ya 139 duniani.
Kung'olewa kwa kipigo cha jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Uganda katika michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kumeiporomosha Tanzania kutoka nafsi ya 127 iliyokuwa mwezi uliopita huku sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Taifa Stars ikiishusha Uganda kwa nafasi mbili kutoka 71 mwezi uliopita hadi nafasi ya 73.
Licha ya kung'olewa kwa kipigo cha jumla ya mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia katika michuano ya CHAN 2016, Kenya imepanda kwa nafasi saba ikishika nafasi ya 116 duniani.
Kutokana na kuporomoka huko, Tanzania ambayo mwezi uliopita ilishuka kwa nafasi 20, sasa ni ya mwisho katika ubora wa soka Afrika Mashariki, Uganda wakiongoza wakifuatwa na Rwanda ambao wamepanda kwa nafasi 16 na kushika nafasi ya 78 duniani, Kenya na Burundi waliopanda kwa nafasi tatu hadi 131.
Argelia wanaendelea kuongoza 10 Bora barani Afrika wakiwa nafasi ya 19 duniani wakifuatwa na Ivory Coast (21), Ghana (25), Tunisia (32), Senegal (39), Cameroon (42), Kongo (47), Cape Verde (52) na Nigeria ambao wameshuka kwa nafasi 14 hadi nafasi ya 57 duniani.
Baada ya kutinga fainali za Copa America, Argentina wameing'oa Ujerumani katika nafasi ya kwanza duniani. Wanafainali hao wa Kombe la Dunia mwaka jana nchini Brazil wanafuatwa na Ujerumani, Ubelgiji, Colombia, Uholanzi, Brazil, Ureno, Romania, England na Wales katika kukamilisha 10 Bora duniani.
Mabingwa wapya wa Copa Amerika, Chile wamepanda kwa nafasi nane na kukwepa hadi nafasi ya 11 duniani kutokana na kufanya vyema katika michuano hiyo mwaka huu, hasa kuifunga Argentina kwenye mechi ya fainali kwa penalti 4-1.
Comments
Post a Comment