YANGA: MWASHIUYA ALIKUWA MCHEZAJI HURU


YANGA: MWASHIUYA ALIKUWA MCHEZAJI HURU
Muro na Mwashibhuya mbele ya waandishi wa habari leo
Jerry Muro (kulia) na Geofrey Mwashiuya wakiwa mbele ya waandishi wa habari leo
Na Bertha Lumala
UONGOZI wa Yanga umesisitiza kuwa ulimsajili kiungo Geofrey Mwashibhuya akiwa mchezaji huru.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya klabu hiyo jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, amesema kuwa Mwashiuya hakuwa na mkataba na klabu yoyote kabla ya kutua Jangwani.
"Kuna maneno mengi yanasemwa juu yetu na usajili wa mchezaji Mwashibhuya. Ukweli ni kwamba kabla ya sisi (Yanga) kumsajili, hakuwa na mkataba na klabu yoyote," amesema Muro na kueleza zaidi:
"Pia taratibu za usajili zinasema kuwa mchezaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza nchini mkataba wake unafika kikomo mara tu ya msimu husika kumalizika.
"Mwashiuya alikuwa hapa kwetu tangu Oktoba mwaka jana, lakini amesaini mkataba wa miaka mitatu hivi karibuni."
Kiungo huyo aliyekuwa amefuatana na Muro katika mkutano na waandishi wa habari, pia amesisitiza hakuwa na mkataba wowote na klabu nyingine klabu ya kutia saini kwa mabingwa haoa mara 25 wa Tanzania Bara.
Kauli ya Yanga imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya uongozi wa Kimondo FC, ambayo Mwashibhuya aliitumikia, kudai kuwa klabu hiyo ya Jangwani haikufuata taratibu stahiki za usajili katika kumnasa mchezaji huyo.
Mwashiuya aliyezaliwa Desemba 27, 1996 jijini Mbeya, alionyesha kiwango kizuri katika mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Yanga dhidi ya SC Villa ya Uganda iliyomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Jumamosi.
SHEREHE ZAZINDULIWA
Katika hatua nyingine, Muro amesema kuwa uongozi wa Yanga umezindua rasmi sherehe za kuadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo ambazo kilele chake kitakuwa Jumamosi kwenye viwanja vya Jangwani jijini.
Amesema Jumamosi kutakuwa na hafla kubwa itakayochagizwa na shrehe za ubingwa wa 25 wa Tanzania Bara.
Yanga ilianzishwa 1935 na kwa sasa ndiyo timu kongwe zaidi nchini inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

 



Comments