TUNAKUKARIBISHA DYLAN KERR, LAKINI….
Na George Mganga
Uzalendo na uvumilivu ni jambo moja lenye uzito na lisilozingatiwa na watu wengi sana, haswa katika tasnia ya wapenda mpira na wadau wa mpira kwa ujumla.
Inachukukua muda mrefu sana kwa Watanzania au watu husika wenye uchu wa mafanikio kuwa na moyo wa subira, hawataki kuwa na mavazi ambayo watayatumia kwa muda mrefu ili kuondoa gharama ya fedha, kununua mavazi mengine ili wavae wapendeze.
Huu ni ugonjwa ambao tunao sisi wazalendo wa lugha ya Kiswahili ama kwa maana nyingine watu wa Afrika Mashariki, ama watu wanaotaka mafanikio ya haraka zaidi bila kuwa na uvumilivu.
Katika harakati na changamoto za maisha kuna kupanda na kushuka, kuna milima na mabonde, kuna hatua mbalimbali za kupitia, kitu ambacho hakiwezi kumwezesha binadamu wa kawaida afike huko anapoelekea kwa wakati mwafaka.
Hakuna asiyejua kuwa kariba, tamaduni na hata tabia ya vilabu vya timu zetu hazipo katika mashindano kwaajili ya kushindana tu bila mafanikio bali kunyanyua vikwapa juu nikiwa na maana ya mataji ndiyo jambo linalozingatiwa.
Vilabu maarufu kama Simba na Yanga havina huruma ya urafiki hata siku moja, na mara nyingi huleta mtafuruku wa uongozi na hata wachezaji pia Kocha pindi mmojawapo anapofungwa katika mechi inayohusisha watani hawa wa jadi.
Klabu za Simba na Yanga kwa sasa zimeshafukuza Makocha wengi tu kuliko vilabu vingine vyote vinavyoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa wakati huu.
Simba ilishawahi kumuajiri Partick Phiri zaidi ya mara mbili lakini hadi leo hii hayupo baada ya kufukuzwa mara 3 tokea aitwe katika awamu tofauti na moja ya vigogo hao.
Yanga pia ni kitu kimoja kutokana na jinsi tangu nianze kufuatilia soka la hapa Tanzania ilishawahi kumfukuza pia Kocha ambaye yupo hivi sasa na hatimaye amerejeshwa tena.
Hii ni kasumba ambayo Dylan Kerr anatakiwa ajiandae nayo kwaajili ya kuja kuondoa kiu ya wapenzi, wadau na mashabiki wa Simba kwa ujumla kwani ni takribani miaka mitatu sasa timu hiyo haijafanya vizuri.
Hakuna asiyetambua kuwa Simba ni klabu kubwa na ipo kwaajili ya kutwaa mataji na sio kushindana, ni moja ya vilabu kama Chelsea, Manchester City, ambavyo huwa havina uvumilivu kabisa pindi Kocha anapoboronga.
Kwa maana hiyo sasa Dylan Kerr hana budi kuja na mbinu itakayomsaidia yeye kuhakikisha kuwa anaipatia matokeo na mataji timu ambayo ilikuwa katika maboresho kwa msimu ulioisha.
Kwa mujibu wa msemaji na hata uongozi wa Simba kwa ujumla ulisikika na kusomeka kuwa hawakuwa na nia ya wao kutwaa kombe la ligi kwa msimu uliopita bali ni kuiandaa timu kwaajili ya msimu ujao ambao ni huu unaotarajiwa kuanza mwezi wa 8.
Kipi anachotakiwa azingatie sasa, ili kuhakikisha anakuwa na nafasi nzuri au maendeleo mazuri ya kuijenga na kuisaidia timu, uhuru pia anatakiwa apewe na uongozi wake na sio swala la kuingilia kazi yake.
Tatizo kubwa linalofanywa na viongozi wa hivi vilabu viwili ni kuingilia madaraka ya mwalimu jambo ambalo halistahili hata kidogo sababu anakosa haki yake ya msingi.
Unapompatia nafasi kiongozi kufanya yale yanayostahili katika kazi yake maalum aliyokubaliwa na umma lazima atatenda kwa ufasaha bila woga na pasipo kupokea vitisho kwa viongozi waliomwajiri.
Natumia nafasi hii kuuomba uongozi wa Simba umpe nafasi Mwalimu huyu katika nyanja zote ili aweze kuitumikia timu vema zaidi.
Mambo ya kumpangia kikosi, kumsajiria wachezaji yashapitwa na wakati sababu haisaidii kuboresha timu hata kidogo.
Ninaandika haya sababu Kocha ndiye anakuwa na mamlaka ya kuiongoza timu na siyo viongozi kwani wao hawana majukumu ya kuingilia mipango ya Kocha.
Twakukaribisha Dylan Kerr lakini kumbuka huku hakuna subira inayovuta kheri pindi unapoenda kinyume na kariba ya soka la vilabu vyetu, kila la kheri katika safari yako ya kuja huku Tanzania.
Kama una maoni yoyote juu ya hiki nilichokiandika wasiliana nami kwa hii namba 0688665508.
Comments
Post a Comment