MANCHESTER UNITED inataka kumfanya Sergio Ramos kuwa miongoni mwa nyota wake wanaolipwa fedha nyingi kwa kumtengea mshahara wa pauni 260,000 kwa wiki, na klabu yake ya Real Madrid imeripotiwa kumwachia aondoke kama atapendezwa na ofa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa, beki huyo mwenye umri wa miaka 29, anataka kuondoka haraka kwa miamba hiyo ya La Liga baada ya mazungumzo ya mkataba mpya kuvunjika na United ina nia ya kumpeleka Old Trafford kwa kumlipa sawa na staa wake Wayne Rooney.
Ramos anaelezwa kutofurahishwa na kitendo cha Real Madrid kuacha mkataba wake kuingia katika miaka miwili ya mwisho, na kuonekana kutokuwa tayari kukubaliana na matakwa yake ya kulipwa dili jipya la pauni 140,000 kwa wiki.
Kwa mujibu wa gazeti la AS la Hispania, United inaaminika kuwa tayari kuweka mezani ofa ya mkataba utakaomwezesha Ramos kulipwa mshahara mara mbili ya ule anaolipwa sasa na Madrid, huku klabu hiyo ya Hispania ikitengewa pauni milioni 21.4 pamoja na De Gea kukamilisha dili litakalokuwa na thamani ya pauni milioni 53.5.
Comments
Post a Comment