MANJI AMTAJA REGINARD MENGI WA IPP KUWA NDIYE MBAYA WA YANGA


MANJI AMTAJA REGINARD MENGI WA IPP KUWA NDIYE MBAYA WA YANGA

SAM_1702

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amesema atajiuzulu wadhifa wa uenyekiti iwapo itabainika kuwa kweli yeye ni fisadi, mwizi na muongo kama ambavyo Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amekuwa akisukuma mashambulizi dhidi yake.

Manji amezungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Yanga, leo na kueleza hayo huku akisisitiza kumtaka Mengi ajitokeze na wakutane kwa ajili ya kufanya mdahalo wa wazi ambao utadhibitisha kuhusiana na tuhuma hizo.

Alisema kuendelea kuiongoza Yanga wakati imethibitika ni fisadi na mwizi, ni utovu wa nidhamu na wanachama wa klabu hiyo watamtilia shaka.

Bilionea huyo ameyasema hayo leo Jumapili, mbele ya wanachama wa klabu hiyo kwenye mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Yanga, makutano ya Mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar.

Manji alifunguka kuwa Mengi amekuwa akimsakama kwa muda mrefu na sasa amesema amechoka.

Manji anadai kilichomchefua zaidi ni habari iliyotoka kwenye Gazeti la Nipashe kuwa kampuni yake ya Farm Equip Tanzania and Quality Garage, ijulikanayo kama QG Engineering ilishindwa kulipa kiasi cha bilioni 9.055 serikalini.

Manji amekanusha taarifa hiyo na kuomba Julai 3, mwaka huu kukutana na mmiliki wa gazeti hilo, Mengi kwenye mdahalo 'live' na kila upande uje na ushahidi wa kutosha kisha Watanzania wapige kura ili muongo na mkweli ajulikane kuliko kuchafuliwa jina.

"Iwapo itabainika kweli mimi ni fisadi, muongo na mwizi, niko tayari kuachi ngazi ya uenyekiti wa Yanga na sitagombea cheo chochote hapa, maana klabu itakuwa inaongozwa na mtu asiye na vigezo sitahiki vya kuwa kiongozi," alisema Manji.

"Watu wanapaswa kujiuliza, mimi ni fisadi ninayejulikana na vyombo vya habari vya IPP tu? Wengine hawaoni hilo? Je, kwa nini IPP pekee ndiyo waone mimi ni fisadi? hapo watu wajiulize," alisema Manji.

Source: Salehjembe



Comments