GEORGE WEAH: MCHEZAJI BORA PEKEE WA DUNIA KUTOKA AFRIKA


GEORGE WEAH: MCHEZAJI BORA PEKEE WA DUNIA KUTOKA AFRIKA

weah

Na Simon Chimbo;

Kama kuna mchezaji, Waafrika tunaweza jivunia ama kutembea kifua mbele katika ulimwengu wa soka ni mwanasiasa wa sasa wa Liberia 'George Tawlon Manne Oppong Ousman Weah'. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liberia anatajwa kua mchezaji bora wa Afrika wa muda wote na pengine wa pekee zaidi barani Afrika kutokana na kuwa mwaafrika pekee kushinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia 'Ballon d'Or'.

Weah alizaliwa Oktoba mosi, 1966 huko Grand Kru, Liberia. Alitangazwa mchezaji bora wa dunia mwaka 1995, huku akishinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mara tatu. Mwaka 2004 aliandikwa katika orodha ya wachezaji 100 bora wa fifa ambao bado wanaishi.

Maisha yake ya mpira

George Weah alitua barani Ulaya mwaka 1988 baada ya kusajiliwa na kocha Arsene Wenger, akiifundisha Monaco kipindi hicho. "Weah ni kipaji cha ajabu. Sijawahi ona mchezaji akijituma kama yeye uwanjani" alikaririwa kocha wa sasa wa Arsenal ya Uingereza, Arsene Wenger

Mwaka 1991 Weah alikua katika kikosi cha Monaco kilichoshinda kikombe cha ligi France Cup. Alijiunga na Paris Saint Germain (1992-1995) akishinda kikombe cha ligi mwaka 1994 na kuwa mfungaji bora wa klabu bingwa Ulaya msimu huo huo wa 1994-1995 akifunga magoli 16 katika mechi 25 alizocheza za Ulaya huku akifunga goli la ajabu dhidi ya Beyern Munich katika michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka barani Ulaya.

Weah alijiunga na Ac Milan mwaka 1995 na kushinda kikombe cha ligi ya Italia 1996 na 1999. Mwaka 1995 alishinda tuzo ya Ballon d'Or na kutangazwa mchezaji bora wa fifa wa dunia. Weah akawa mchezaji maarufu zaidi katika kikosi cha Milan baada ya kufunga goli la uwezo binafsi, 'solo goal' dhidi ya Verona katika dimba la San Siro akiwapiga chenga wachezaji saba kabla ya kufunga.

Baada ya kuondoka Milan januari 2000, George Weah alijiunga Chesea, Manchester City na Olympique Marseille kwa mafanikio ya haraka, kabla ya kuondoka Marseille mwezi Mei 2001 akielekea Al Jazira fc ya Falme za kiarabu, ambako alicheza na kustaafu soka lake mwaka 2003.

Pamoja na mafanikio makubwa katika ngazi ya klabu, Weah alishindwa kufanya hayo akiwa na timu ya taifa ya Liberia. Alifanya kila alichoweza katika timu ya taifa katika kucheza, kufundisha na kuiwezesha kifedha lakini akishindwa kuisaidia kufuzu hata mara moja katika fainali za kombe la dunia. Huku wakishindwa kwa pointi moja tu kufuzu katika fainali za kombe la dunia zilizo fanyika 2002.

Mchezaji bora wa dunia wa fifa 1995

Weah alitangazwa mchezaji bora wa dunia wa Fifa mwaka 1995, na kua mchezaji pekee wa Afrika kushinda tuzo hiyo. Akiwa ni mchezaji wa tano kupokea tuzo hiyo tangu zilipoanza kutolewa.

Mchezaji bora wa Afika wa mwaka 1989, 1994 na 1995

Weah alishinda pia tuzo za mchezaji bora wa mwaka wa Afrika 1989 akiwa na Monaco, 1994 akiwa Paris Saint Germain na 1995 akiichezea Ac Milan, mwaka ambao alishinda tuzo zote mchezaji anaweza kushinda. Huku mwaka 1989 ikiwa ni tuzo yake ya kwanza kubwa kutwaa na kuamua kurudi nayo nyumbani kusherehekea nchi nzima.

Mchezaji bora wa Ulaya 1995

Mwaka huo wa mafaniko zaidi ya kijana huyo wa Afrika alitangazwa mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or (mchezaji bora wa Ulaya) akiwa mwaafrika wa kwanza kushinda tuzo hiyo. Waandishi wote wa  habari za michezo duniani walimpigia kura kama mchezaji bora zaidi wa Ulaya wa muda huo. Baada ya kushinda tuzo hiyo, George Weah alimshukuru kocha Arsene Wenger kwa kuamini kuwa ndiye aliyemfanya afikie mafanikio hayo.

Mchezaji bora wa karne wa Afrika

Weah alitangazwa mchezaji bora wa karne wa bara la Afrika baada ya kupigiwa kura na waandishi wa habari za michezo. Huku mbrazil Pele akishinda kuwa mchezaji bora wa karne wa bara la Amerika kusini wakati Johan Cruyff akishinda kwa bara la Ulaya.

UTATA

George Weah alijikuta kwenye matatizo na kufungiwa mechi sita za michuano ya Ulaya baada ya kumpasua pua mlinzi wa Porto fc na timu ya taifa ya Ureno  Jorge Costa mnamo Novemba 20, 1996 katika sehemu ya nje ya vyumba vya kubadilishia nguo 'player's tunnel' baada ya matokeo ya sare kati yake ya Ac Milan na Fc Porto. Weah alitoa sababu za yeye kumpiga na kumjeruhi beki huyo wa Porto kua ni kauli za kibaguzi 'racist taunts' kutoka kwa beki huyo katika mechi hiyo ya usiku wa Ulaya.

Lakini mlinzi huyo Jorge Costa alikanusha vikali madai hayo na kukwepa adhabu baada ya kukosekana kwa ushahidi wa tuhuma hizo. Baadae Weah alijaribu kumuomba msamaha Jorge Costa kwani alimuumiza na kusababisha akae nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki tatu, lakini mlinzi huyo hakuwa tayari kumsamehe Weah. Pamoja na tukio hilo, George Weah alitunukiwa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu duniani 'Fifa fair play award' na Fifa mwaka 1996.

 Maisha yake nchini Uingereza

Januari 11 mwaka 2000 Weah alisajiliwa na Chelsea akitokea Ac Milan kwa mkopo, mkataba uliokua ukimuweka klabuni hapo kwa msimu wa 1999-2000. Maisha yake nchini Uingereza yalikua ya mafanikio hususani akiwa na Chelsea baada ya kufunga goli katika mechi yake ya kwanza dhidi ya mahasimu wakubwa wa Chelsea 'London derby' Tottenham Hotspurs na kuendelea kufunga magoli zaidi dhidi ya Wimbledon na Liverpool.

Aliifungia Chelsea pia magoli mawili katika fainali chama cha soka England FA cup, akifunga magoli muhimu dhidi ya Leceister na Gillingham na kuipa ubingwa timu yake hiyo katika ushindi wa bao moja bila katika fainali. Kocha wa Chelsea wakati huo Gianluca Vialli hakuwa kamsaini kwa mkataba wa kudumu na hivyo Weah kujiunga na Manchester city kwa mkataba wa miaka miwili, huku akilipwa dola 30000 kwa wiki. Aliichezea city mechi 11 na kufunga mara nne na kuamua kuondoka baada ya kuwekwa nje mara nyingi na kocha Joe Royle.

Timu ya taifa

Weah aliichezea Liberia michezo 60 katika kipindi cha miaka 20 na kufunga magoli 22. Amekua ni mchezaji muhimu wa Liberia huku akiwa kocha kipindi fulani na kuwawezesha kifedha.

 Ageukia siasa

Baada ya kuisha kwa vita vya pili vya ndani ya nchi 'second Liberian civil war' Weah akatangaza nia yake ya kuwania uraisi wa nchi yao katika uchaguzi wa mwaka 2005 akiunganisha chama cha Congress for democratic change. Pamoja na kuwa maarufu zaidi nchini Liberia, upinzani ulitumia kampeni zake kumkosoa kwa kukosa elimu ya darasani kama kikwazo cha yeye kuiongoza nchi ukilinganisha na mpinzani wake mama Ellen Johnson Sirleaf ambae alisoma katika chuo cha Harvard.

Wachambuzi pia wa masuala ya kisiasa nchini Liberia walimzungumzia Weah kama mwanasiasa asie na uzoefu, huku mama Ellen akiwahi kuwa waziri wa fedha kuanzia miaka ya 1970 huku akifanya kazi katika benk ya dunia. Weah pia alizua maswali kutokana na awali kupewa uraia wa ufaransa akiwa Paris Saint Germain kama mchezaji. Mahakama ilimuondolea vikwazo hivyo vyote na kumruhusu agombee. Alitikisa nchi nzima kutokana na umaarufu wake lakini matokeo ya mwisho ya uchaguzi yalimpa ushindi mama Ellen Sirleaf kwa ushindi wa 59.4% dhidi ya 40.6% alizopata George Weah.

Matokeo hayo ya uchaguzi yalisababisha vurugu kutoka kwa wafuasi wa Weah ambao hawakuridhishwa na taratibu za uchaguzi pamoja na matokeo. Lakini baadae wadau wa masuala ya siasa nchini Liberia waliwaomba wafuasi wa Weah wakubali matokeo kwani uchaguzi ulikua halali. Kasha bibi Ellen akatangazwa raisi nchini Liberia. Suala la elimu lilikua ni ishu nchini Liberia kutoka kwa upinzani na hata kumfanya ashindwe tena kumzuia bibi Ellen Sirleaf katika uchaguzi wa mwaka 2011. Weah akachaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa chama cha Congress for democratic change.

 

0712 439356



Comments