TFF imetudanganya tena mchezaji bora VPL

ngassaNgassa pekee ndiye mchezaji aliyetwaa tuzo kihalali

'Tangu kuanza kutolewa kwa tuzo ya mchezaji bora waVPL Septemba mwaka jana, ni mchezaji mmoja pekee aliyetwaa tuzo hiyo kihalali kama utaratibu sahihi wa kumpata mchezaji bora wa mwezi ungelifuatwa.'

 

MACHI 23 mwaka huu nilieleza namna Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilivyompoka tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa mwezi Februari mshambuliaji wa kimataifa wa Stand United kutoka Nigeria, Abasirim Chidiebere.
Nilieleza namna nia njema ya kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania kuhakikisha soka la Bara linakua, inavyodidimizwa na kitendo cha TFF kuachia utaratibu mbovu wa kumpata Mchezaji Bora wa Mwezi wa VPL uendelee.
Kwa wanaofuatilia kwa kina VPL msimu huu, watakubaliana na mimi kwamba tangu tuzo hizi zianze kutolewa Septemba mwaka jana, ni mchezaji mmoja tu, Mrisho Ngasa, aliyetwaa tuzo hiyo kihalali kama taratibu sahihi katika kumpata Mchezaji Bora wa Mwezi zingelifuatwa.
Mchezaji Bora wa Mwezi, angalizo kwa jopo la makocha la TFF, anapaswa kuwa yule ambaye alitoa mchango mkubwa uwanjani katika kuipa timu yake mafanikio ambayo ama hayakufikiwa na timu nyingine, au hayakupitwa na washindani wao katika kipindi hicho.
Chidiebere ndiye aliyepaswa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Februari kutokana na mchango wake mkubwa katika kikosi cha Stand United.
Ndani ya mwezi huo timu hiyo ya mjini Shinyanga ilicheza mechi tano ikifungwa 2-1 ugenini dhidi ya Ruvu Shooting, ikatoka sare ya bao moja (1-1) ugenini dhidi ya Ndanda FC kabla ya kushinda nyumbani 4-1 dhidi ya Mgambo Shooting, 1-0 dhidi ya Simba na 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Katika mechi hizo ilizokusanya pointi 10, Chidiebere alifunga mabao sita na kuwa mchezaji pekee wa VPL aliyefunga mabao mengi zaidi mwezi huo huku Stand ikikwea kutoka nafasi ya 12 hadi nafasi ya saba katika msimamo wa ligi.
Yanga ndiyo timu iliyokusanya pointi nyingi zaidi Februari (pointi 13) ikitoka suluhu dhidi ya Ndanda FC na kushinda 1-0 dhidi ya Coastal Union, 2-0 Mtibwa Sugar, 3-0 Tanzania Prisons na 3-1 Mbeya City.
Jopo la makocha la TFF lingelimchagua mmoja wa wachezaji wa Yanga kutwaa tuzo hiyo, pengine lingelieleweka kwa umma, lakini mawinga wake Mrisho Ngasa na Simon Msuva waliong'ara katika kikosi cha wanajangwani mwezi huo, hawakuifikia idadi ya mabao ya Chidiebere. Walifunga mabao matatu kila mmoja katika mechi zote tano.
Yanga ilifuatwa na Stand kwa kufanya vizuri mwezi huo ikikusanya pointi 10 ikifuatwa na na Kagera Sugar (9), Ndanda FC (8), Simba (7), Ruvu Shooting, Azam FC na Coastal (6), Mbeya City na Mgambo (3), Prisons (2), Mtibwa, JKT Ruvu na Polisi Moro wakiambulia pointi moja tu kila mmoja.
Kikosi cha Coastal Union kilichokuwa chini ya kocha mkuu Mkenya James Nandwa kilichotoa mchezaji bora wa Februari,Godfrey Wambura,  kilikusanya pointi sita mwezi huo kikifungwa 1-0 nyumbani dhidi ya Yanga, suluhu dhidi ya Simba na Mbeya City (Tanga), kikapoteza 0-1 dhidi ya  Ndanda FC (Mtwara) kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Mgambo (Tanga).
Katika mechi hizo tano Wambura (aliyepewa tuzo ya Chidiebere) hakufunga kwani bao lao pekee la mwezi mzima katika kikosi chao lilifungwa na Lutimba Yayo.
Licha ya kutoa ufafanuzi wa namna jopo maalum la makocha la TFF linavyoteleza katika kumpata mchezaji bora wa kila mwezi wa VPL, somo linaonekana halijaingia baada ya Ijumaa shirikisho hilo kumtangaza winga wa kushoto James Mwasote wa Police Morogoro kuwa ndiye mchezaji bora wa mwezi Machi.
Mwasote anakuwa mchezaji wa pili wa kikosi cha Police Moro kutwaa tuzo hiyo 'kwa kubebwa' na TFF baada ya mshambuliaji anayekipiga kwa mkopo kutoka Yanga Said Bahanunzi kutawazwa mkali wa Januari.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano, Baraka Kizuguto, ikiwa na kosa lililomtaja Mwasote ni mchezaji wa Tanzania Prisons, jopo maalum la makocha limemtangaza pia winga Mrisho Ngassa wa Yanga kuwa mchezaji bora wa Aprili akiwapiku Amos Edward, Frank Domayo wa Azam FC na Emmanuel Okwi wa Simba. 
Sehemu ya taarifa hiyo inasomeka: "Mchezaji James Mwasote Ambrose wa timu ya Tanzania Prisons (Police) amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Machi 2015 kufuatia kuwapiku wachezaji wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo." 
Sina wasiwasi na tuzo aliyopewa mchezaji wa zamani wa Kagera Sugar, Azam FC na Simba, Ngassa, lakini hii ya Mwasote sikubaliani nayo kutokana na sababu kuntu zilizojikita katika misingi ya kitakwimu. Ikumbukwe kuwa soka ni takwimu.

MCHEZAJI BORA MACHI
JKT Ruvu inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Felix Minziro, ndiyo timu iliyocheza mechi nyingi zaidi Machi (mechi tano) wakati Kagera Sugar inayonolewa na Mganda Jackson Mayanja ndiyo timu iliyocheza mechi chache zaidi mwezi huo (mechi mbili).
Azam ndiyo timu iliyokusanya pointi nyingi zaidi Machi (10) ikitoka sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City baada ya kushinda 1-0 mfululizo dhidi ya JKT Ruvu, Ndanda FC na Coastal Union.
Yanga na Simba walishika nafasi ya pili  wakikusanya pointi tisa, mabingwa Yanga wakifungwa 1-0 dhidi ya Simba na kushinda mfululizo 2-1 dhidi ya Kagera Sugar, 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting na 3-1 dhidi ya JKT Ruvu.
Mgambo walifuata wakikusanya pointi saba wakifuatwa na City (6), JKT Ruvu na Prisons (5), Ndanda na Mtibwa (4), Coastal, Ruvu Shooting na Police (2), Kagera (1), Stand United (0).   
Kwa takwimu hizi, ni wazi kwamba mchezaji bora wa Machi wa VPL alipaswa kutoka timu iliyofanya vizuri mwezi huo, yaani Azam au Simba na Yanga ambazo zilizidiwa pointi moja kimafanikio na mabingwa hao wa msimu uliopita.
Police Morogoro ambayo imetoa mchezaji bora (Mwasote), imeambualia pointi mbili kati ya 12 katika mechi zote nne ilizocheza ndani ya mwezi huo.
Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Adolf Richard aliyetimuliwa, kilifungwa 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar (Manungu), kikatoka suluhu dhidi ya Ruvu Shooting (Jamhuri), kikapoteza 1-0 nyumbani dhidi ya JKT Ruvu kabla ya kutoka suluhu ugenini jijini Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons.
Bao pekee la mwezi huo la Police Morogoro lilifungwa kwa penalti na Bahanunzi dakika ya 40 huku Mtibwa wakipata mabao kutoka kwa mshambuliaji Ally Shomari na beki mkongwe Said Mkopi.

MCHEZAJI BORA APRILI
Mabingwa mara 25 wa Tanzania Bara, Yanga ndiyo waliokusanya pointi nyingi zaidi Aprili (15) wakishinda mechi zote walizocheza wakifuatwa na Simba (9), Azam na Prisons (8), Mbeya City na Stand United (7), Kagera Sugar na Ruvu Shooting (6), Mtibwa (5), Mgambo, Coastal, JKT Ruvu na Police (4) na Ndanda (2).
Kwa kutumia kigezo kilekile kinachozingatiwa kimataifa, mchezaji bora wa Aprili wa VPL anapaswa kutoka Yanga ambayo ilizifunika timu nyingine zote za ligi hiyo ndani ya mwezi huo.
Amissi Tambwe na Msuva waliotisha kwa kufumania nyavu ama mchezaji yeyote wa Yanga aliyesaidia timu hiyo ya Jangwani kukusanya pointi 15, kufunga mabao 23 na kufungwa mabao manne pekee katika mechi zote tano za mwezi huo, anastahili kutwaa tuzo hiyo.
Jopo la makocha la TFF limemtangaza Ngassa, ambaye binafsi ninaamini ni mtu sahihi kubeba tuzo hiyo kutokana na mchango mkubwa katika kikosi cha wanajangwani kipindi hicho.
Ingawa Ngasa amefunga bao moja tu katika mechi zote hizo, alipika magoli mengi ambayo Msuva na Tambwe walifunga.
Mathalani, katika mechi dhidi ya Police Morogoro waliyoshinda 4-1 Jumatatu, Ngassa alipika mabao yote matatu yaliyofungwa na Tambwe (2) na Msuva.
Kinara wa mabao VPL kwa sasa, Msuva ndiye aliyepika bao la kwanza la mechi hiyo lililofungwa na Tambwe dakika ya 41 ya mchezo.

Ninaishauri Kamati ya Utendaji ya TFF kukaa na jopo lao la makocha na kuangalia upya vigezo wanavyovitumia kumpata Mchezaji Bora wa Mwezi wa VPL kwa vile utaratibu wa sasa hauwiana na utaratibu unaotumika sehemu mbalimbali duniani.
Wachezaji Bora wa VPL
Jina    Timu    Mwezi
Antony Matogolo    Mbeya City    Sept
Salum Abubakar    Azam FC    Oktoba
Rashid Mandawa    Kagera   Novemba
Joseph Mahundi    Coastal   Desemba
Said Bahanunzi    Police   Januari
Godfrey Wambura    Coastal    Febr
James Mwasote    Police    Machi
Mrisho Ngassa    Yanga        Aprili

*Imeandikwa na Sanula Athanas, mwandishi wa michezo mwandamizi wa NIPASHE

 

CHANZO: NIPASHE



Comments