Tambwe aeleza kinachoendelea kwasasa Burundi



Tambwe aeleza kinachoendelea kwasasa Burundi

AmissTambwe2

WAKATI imeripotiwa kwamba rais wa Burundi, Piere Nkurunziza ametua jana mjini Bujumburu kutoka Dar es salaam Tanzania, hali ya utulivu imeanza kurudi nchini humo.

Jana Nkurunziza ali-tweet akithibitisha kurejea nchini kwake na kuwashukuru wanajeshi watiifu na polisi kwa uvumilivu wao wa kuipigania serikali iliyopo madarakani.

Mkuu wa jeshi la Burundi amesema jaribio la mapinduzi lililofanywa na Jenerali Godefroid Niyombare halijafanikiwa.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi na Yanga, Amissi Tambwe aliyepo eneo la Akamba nchini humo kwa mapumziko baada ya ligi kuu soka Tanzania bara kumalizika mei 9 mwaka huu, amezungumza na mtandao huu kueleza hali ya mambo inavyokwenda.

" Mambo yametulia, televisheni ya taifa inaonesha vipindi vya kawaida kama kawaida. Serikali ya mwanzo bado ipo madarakani na ndio ilizua hizo vurugu, lakini sahizi mambo shwari, hakuna vurugu tena". Amesema Tambwe na kufafanua: "Mchezo wa soka unakutanisha watu, unawaweka watu pamoja na kuleta amani, shughuli za mpira zinaendelea, wakati nakuja jana (juzi) nimepita maeneo kadhaa na kuona watu wanaendelea kucheza kama kawaida".

Tambwe ameshika nafasi ya pili kwa ufungaji wa magoli (mabao 14) msimu wa 2014/2015 nyuma ya mfungaji bora wa msimu wa 2014/2015 aliyetikisa nyavu mara 17, Simon Msuva.

Msimu wa 2013/2014, Tambwe akiichezea Simba aliibuka mfungaji bora kwa kutikisha nyavu mara 19 na anatajwa kuwa mshambuliaji hatari zaidi kwa misimu miwili mfululizo.



Comments