Sepp Blatter aogopa Kuingia Marekani Kwa Sababu ya uchunguzi wa FBI


Sepp Blatter aogopa Kuingia Marekani Kwa Sababu ya uchunguzi wa FBI

blatter-1363184897

Imeripotiwa kuwa Rais wa FIFA, Sepp Blatter anaogopa kuingia Marekani kutokana na uchunguzi wa FBI unaoendelea hivi sasa kuhusu uongozi wa FIFA kuzizawadia nchi za Russia na Qatar kuandaa Kombe la Dunia 2018 na 2022.

Kupitia kipindi cha masuala ya uchunguzi cha  ESPN  kiitwacho  E:60, Jumanne hii, kilimwangalia Blatter. Kama walivyoripoti kupitia akaunti yao ya mtandao wa Twitter, inaonekana Blatter, 79, hataki kuingia Marekani kwa sababu ya uchunguzi juu ya rushwa na ufisadi endapo kama vilitumika katika kuzawadia nchi husika kuandaa Kombe la Dunia.

Lakini, kama ilivyoripotiwa na Bryan Swanson wa Sky Sports, FIFA ilijibu haraka tuhuma hizi. Kupitia akaunti ya Bryan Swanson ya twitter, @skysports_bryan, twiti hiyo ilisema hivi, [FIFA: 'Si kweli kabisa' kudai kuwa Sepp Blatter kakataa kwenda Marekani 'kwa sababu ya maombi ya FBI']

Hapo kabla, FIFA haikuona ushahidi wowote juu ya rushwa au makosa  yoyote katika uchunguzi wake. Lakini FBI iliamua kuendelea na uchunguzi wake, ambao una miaka mitatu sasa.

Inategemewa FBI itaomba kuona ripoti fupi ya Michael Garcia iliyotolewa  kupitia BBC Sport kwa kuwa yeye ndiye aliyeendesha uchunguzi mzima wa FIFA.

Lakini pia kupitia Charles Sale wa gazeti la Uingereza, Daily Mail aliripoti, "UEFA imezidi kuwashuku wanasheria wa FIFA kuwa watabadilisha ripoti ya Michael Garcia ili kumlinda Rais Sepp Blatter" wakati ripoti mpya itakapotolewa hapo baadaye.

Sale anaamini Blatter kaingia Marekani mara moja tu tangu kura ya kuandaa Kombe la Dunia ilipopigwa mwaka 2010. Anasema, "Blatter hataki kuulizwa maswali" juu ya mambo ya ufisadi na rushwa. Sale pia alithibitisha kuwa Chuck Blazer, mwanachama wa zamani wa FIFA, anatumiwa kama mtoa habari kwa kazi hiyo ya FBI.

Hapo kabla, kipindi cha ESPN kilirushwa hewani mahsusi kwa ajili ya mazingira yasiyo ya kibinadamu kwa wale wanaofanya kazi kwenye viwanja na miundombinu itakayotumika kwa ajili ya Kombe la Dunia, mwaka 2022.

Blatter amebaki kuwa Rais wa FIFA kwa miaka 17 na bado amepanga kugombania kwa mara yake ya mwisho katika uchaguzi wa mwaka huu.

Anategemewa kugombania kiti hicho na Prince Ali bin al-Hussein wa Jordan, Michael van Praag wa Uholanzi na mchezaji wa zamani wa Ureno, Luis Figo. Kama kituo cha habari, BBC kilivyoripoti, wapinzani hao wote watatu walitegemewa kuja na "mbinu moja", ambayo ingelenga kumfanikisha mgombea mmoja kati yao ili tu kumwangusha  Blatter, lakini hilo  limeshindikana.

Owen Gibson wa gazeti la Uingereza, Guardian aliripoti "Blatter anabaki kuwa mgombea mwenye nguvu" na atashinda kwa mara nyingine tena.



Comments