'Nonga ameifungia City mabao manne VPL msimu huu.'
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
MSHAMBULIAJI Paul Nonga wa Mbeya City FC, amezitosa ofa za Simba na Yanga na kuamua kuendelea kuitumikia timu hiyo ya Manispaa ya Jiji la Mbeya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Nonga, mchezaji wa zamani wa JKT Oljoro, amekaririwa katika mtandao ramsi wa City akieleza kuwa ana uhakika wa kuwa sehemu ya kikosi cha Juma msimu ujao licha ya kuwapo kwa ofa nyingi kutoka timu mbalimbali zinazokuwa zinahitaji huduma yake zikiwamo Simba na Yanga.
"Hata kabla ya msimu kumalizika kulikuwa na ofa nyingi kutoka timu mbalimbali ambazo zilionesha nia ya kutaka huduma yangu. Binafsi ninashukuru hilo kwa sababu inaonesha kazi yangu inakubalika, tayari nimeshafanya mazungumzo na City na yako sehemu nzuri. Kwa kifupi hakuna shaka tena juu ya mustakabli wangu ndani ya kikosi. Nia yangu ni kubaki hapa kwa misimu mingi zaidi, nina furaha na maisha ya hapa," amesema Nonga.
Aidha, Nonga aliyekuwa mwiba kwa Simba walipoweka rekodi ya kuwa timu pekee iliyopata pointi zote sita kutoka kwa Simba msimu huu wakiipa kipigo cha mabao 2-0 jijini Mbeya Aprili 18, amesema ana shauku ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara akiwa na kikosi cha City na kuiwakilisha nchi kayika michuano ya kimataifa.
"Ninatamani kutwaa ubingwa wa ligi nikiwa na City, hili linawezekana maana tumeshiriki ligi misimu miwili kwa mafanikio, ninafikiri huu ni wakati wetu sasa kufanya makubwa zaidi. Ninaamini timu itakuwa bora zaidi msimu ujao," amesema.
Mshambuliaji huyo aliyemaliza msimu wa 2014/15 akiwa ameifungia timu yake mabao manne, amesema bado ana deni kubwa kwa mashabiki wa City ambao amedai wana kiu ya kuona timu yao inafungua ramani nyingine kwenye michuano ya kimataifa.
Comments
Post a Comment