Mzee Famau amuita mwenyekiti wa soka Tanga ‘Mafia’


Mzee Famau amuita mwenyekiti wa soka Tanga 'Mafia'
coastal
NA MWANDISHI WETU,TANGA.
MWANACHAMA mmoja wa zamani wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga,Omari Famau amemuita Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tanga(TRFA) ,Said Soud 'mafya' kutokana na uwezo aliokuwa nao wa kuzipandisha na kuzishusha klabu za soka mkoani hapa.
Mwanachama huyo anayejulikana kwa jina la Omari Famau alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa dharura wa wanachama ambao ulikuwa na agenda kuu ya kuwapitisha wanachama walioomba uanachama ambao walikuwa wamefuata taratibu zote na hivyo mkutano huo kuwapitisha.
Mkutano huo uliokuwa na wanachama wapatao 92 kwa pamoja waliazimia kuwapatisha wanachama hao ambao walikuwa wakiomba uanachama kwa muda mrefu wakati kwa wale ambao waliomba siku za hivi karibuni wajaze fomu na kupitishwa nao.
Katika mkutano huo kulizuka mvutano mkubwa baina ya wanachama wenyewe kwa wenyewe baada ya mwanachama mwenzao huyo, Famau kusimama na kusema kuwa Mwenyekiti huyo ni mafya na wanachama na wapenzi wasilete mchezo naye kwa sababu anauwezo wa kufanya jambo lolote analolitaka lifanyike.
"Mimi nawaambie ndugu zangu wanachama msicheze na Said Soud pamoja na watu wenye pesa kwa sababu yeye ni mafya anaweza kuishusha Coastal Union na kuipandisha daraja hivyo muweni makini sana na kiongozi huyo kwa sababu sio mtu ambaye anapenda mchezo mchezo "Alisema Famau.
 Hata hivyo mzee huyo aliwataka wapenzi na wanachama wa klabu ya Coastal Union wasifanye mchezo na watu wenye pesa kwa sababu wataanguka kwa sababu wanaweza kufanya jambo lolote kupitia fedha zao waliokuwa nazo. 
Baada ya kutokea hali hiyo kuliibuka mvutano mkubwa ambao ulidumu kwa kipindi cha nusu saa kabla ya kutulizwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ahmed Mgoyi ambaye  alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Mkutano huo.
"Ndugu zangu wanachama tuweni watulivu ili kulimaliza jambo hili kwa wakati na tulifikie muafaka la sivyo tutakaa hapa mpaka usiku hivyo nawataka tutumie busara zetu kufanikisha mkutano wetu uende vizuri "Alisema Mgoyi ambaye alifanikisha kutuliza mvutano huo.
Awali akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tanga,Said Soud alisema kuwa klabu ya Coastal Union ina uwezo mkubwa wa kupata ubingwa msimu ujao iwapo wapenzi na wanachama watakuwa na mshikamano ili kufikia malengo hayo.
"Ndugu zangu wana Coastal Union tusibaguane tushikamane kuhakikisha msimu ujao tunachukua ubingwa wa Ligi kuu Tanzania bara kwani hilo jambo linawezekana kikubwa ni ushirikiana  "Alisema Mwenyekiti huyo.


Comments