KATIBU mkuu wa kamati ya uchaguzi ya Yanga, Francis Kaswahili jana amekaririwa na vyombo vya habari akisema uchaguzi mkuu wa Yanga SC utafanyika Julai 12, mwaka huu katika ukumbi ambao utatajwa baadaye.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa fomu za wagombea zitaanza kutolewa Mei 17, mwaka huu kwa kuzingatia ratiba.
"Jambo hili ni la kikatiba na wala halina mjadala, tunataka Yanga iwe na viongozi ambao watatokana na utashi wa Wanayanga ni matumaini ya kamati ya uchaguzi kwamba hapatatoka mtu mwingine wa kutaka kuvunja misingi ya katiba". Kaswahili alikaririwa na Bin Zubeiry.
Lakini katika hali ya kushangaza, jioni ya leo mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Yanga, Mwanasheria, Alex Mgongolwa ameibuka na kusema kwa mujibu wa katiba ya Yanga, mwenye wajibu wa kutangaza uchaguzi ni mwenyekiti na sio katibu mkuu ambaye hajui kama ni Francis Kaswahili.
"Kwa mujibu wa katiba, mikutano ya namna hiyo lazima iweze kuratibiwa na sekretarieti, halafu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ndiye anaitisha mkutano mkuu. Kwa mujibu wa katiba za wanachama wa TFF, katibu hawezi kuitisha mkutano wa uchaguzi na pia sina hakika kama yeye ndiye katibu mkuu kwasababu kikatiba katibu mkuu lazima atoke kwenye sekretarieti, nayeye (Kaswahili) sio mjumbe, hana mamlaka yoyote". Mgongolwa amekaririwa na kituo cha redio cha E-fm usiku wa leo.
Mgongolwa amesisitiza kuwa mkutano aliotangaza kaswahili ni batili na hana mamlaka ya kuitisha wala kutangaza huo mkutano.
Hata hivyo kuhusu uchaguzi wa Yanga, Mgongolwa amesema:"Taarifa ambazo nimezipata na ninasubiri mawasiliano kutoka sekretarieti ni kwamba kamati Yangu itakutana wiki ijayo kupanga tarehe ya uchaguzi mkuu wa Yanga".
Comments
Post a Comment